Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema hatua ya wadau wa afya kuweka kambi za matibabu Zanzibar, itasaidia kuondoa matatizo ya afya yanayowakabili wananchi.
Akizungumza na ujumbe
wa watendaji wa hospitali ya Kitengule, kutoka Dar es Salaam, ofisini kwake
Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi, Mama Mariam amesema hatua hiyo ni utekelezaji
wa mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwafikishia huduma za
matibabu wananchi wake maeneo karibu na makaazi yao.
Amesema hatua hiyo
pia inaonesha kuwajali wananchi kwenye suala zima la afya na kueleza kufarijika
kwake baada ya watendaji hao kutambua fursa za matibabu kupitia sekta ya utalii
ambapo itasaidia zaidi kuongeza idadi ya wageni kwa kuwa na uhakika wa matibu.
Mkurugenzi mkuu wa
taasisi hiyo ya ZMBF, bi Fatma Fungo ameupongeza ujumbe huo na kuushukuru kwa kuwapatia
vifaa vya kitabibu vikiwemo vya uchunguzi wa maradhi na kueleza kwamba vitasaidia
kuendesha huduma za kambi za matibabu pamoja na kampeni za afya zinazoratibiwa
na ofisi hiyo.
Akizungumza kwa niaba
ya ujumbe wa hospitali ya Kitengule, Mkurugenzi wa huduma za afya Dk. Restuta
kibasa amesema, wamefurahishwa na muitikio wa wananchi waliokuja na kupata
huduma zikiwemo za uchunguzi na matibabu kwa waliogunduliwa na matatizo mbali
mbali.
Jumla ya wananchi 360
walifikiwa kupata huduma za matibabu kupitia kambi iliyoendeshwa na hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Dar-es Salaam huko hospitali ya Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja
ambako wagonjwa wapatao 104 walipatiwa matibabu.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment