Habari za Punde

Serikali yaimarisha huduma za upasuaji Kituo cha Afya Kisorya, Bunda

Wakazi wa Kijiji cha Kisorya wakiwemo wanawake wajawazito katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wameondokana na adha ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma za afya hususani upasuaji baada ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kuboresha Kituo cha Afya Kisorya.

Awali wakazi hao walilazimika kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 42 hadi Kibara na Kasahunga wilayani Bunda ama kuvuka maji katika Ziwa Victoria hadi Nansio wilayani Ukerewe kufuata huduma za afya hususani wakati wa kujifungua.

Mmoja wa akina mama katika Kijiji hicho, Kasenda Kaguba amesema maboresho katika Kituo cha Afya Kisorya yaliyojumuisha vifaa tiba na uwepo wa madaktari wawili pamoja na manesi wanane umewaondolea adha ya upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo ya upasuaji ambayo haikuwepo tangu Kituo hicho kipande hadhi kutoka Zahanati mwaka 2018.

Kaguba amesema mwezi Aprili mwaka 2021 alifika katika Kituo cha Afya Kisorya kujifungua watoto mapacha ambapo mtoto wa kwanza alijifungua salama lakini akakumbana na uchungu pingamizi kwa mtoto wa pili na kulazimika kupelekwa katika Kituo cha Afya Kibara na kujifungua kwa upasuaji.

Kutokana na changamoto hiyo, mwezi Disemba mwaka 2022 Serikali ilipeleka mashine ya usingizi, mashine ya oksjeni, kitanda cha upasuaji ambapo kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH iliwajengea uwezo watoa huduma katika Kituo cha Afya Kisorya hatua iliyosaidia kuanza kutoa huduma za upasuaji katika Kituo hicho.

Jitihada hizo zimewanufaisha wakazi wa Kijiji cha Kisorya wakiwemo wanawake wajawazito kupata huduma za afya katika Kituo hicho akiwemo Kabuga ambaye Disemba 30, 2022 alijifungua kwa upasuaji katika Kituo cha Afya Kisorya ikiwa ni mara ya kwanza huduma hiyo kutolewa katika Kituo hicho.

Akizungumzia maboresho hayo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisorya, Dkt. Hemedi Hassani amesema tangu huduma ya upasuaji ianze kutolewa katika Kituo hicho Disemba mwaka jana, zaidi ya wanawake 20 wamejifungua katika Kituo hicho, kati yao watano wakijifungua kwa upasuaji.

“Wananchi pia wameongeza imani ya kuja hapa kupata huduma za afya ambapo idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 45 hadi 50 kwa siku na kufikia 80 hadi 100 kwa siku. Tunaishukuru Serikali kwani kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH imetujengea uwezo, sasa tuna uzoefu wa kutoa huduma bora ikiwemo upasuaji” amesema Dkt. Hassani.

Naye Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini, Hellen Magare amesema jitihada za Serikali na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH zimesaidia kiwango cha ubora wa huduma kwa Halmashauri hiyo kuongezeka kutoka asilimia 3.5 hadi 4.1 ambapo lengo ni kufikisa asilimia 5 ambazo ni kipimo cha juu kwa Halmashauri kwa utoaji huduma bora za kitaifa.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana vyema na wadau wa afya hususani mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH na kuboresha huduma za afya katika Halmashauri yetu, jitihada hizi zitasaidia kufikia asilimia tano za ubora katika utoaji huduma za afya” amesema Magare.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabrone Masatu amesema mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH umesaidia kuwajengea uwezo wataalamu pamoja na kuimarisha huduma za afya ikiwemo upasuaji katika Vituo 30 vya afya na hospitali 18 mkoani Mara.

Kwa Mkoa wa Mara, mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH umesaidia kupunguza vifo vya uzazi kwa akina mama kutoka 46 kwa zaidi ya wanawake elfu 90 waliojifungua mwaka 2022 hadi kufikia vifo 32 kati ya wanawake zaidi ya elfu 60 waliojifungua hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2023.

Jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Kisorya Wilaya ya Bunda mkoani Mara zimezaa matunda kwa ushirikiano wa karibu na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya ya mama, mtoto na vijana balehe ukitekelezwa katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga, Simiyu, Tabora , Katavi, Manyara, Dodoma, Tanga na Dar es salaam kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022/27 kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na kutekelezwa na shirika la JHPIEGO kama mdau mkuu.

Mashirika mengine yanayoshirikiana na JHPIEGO kutekeleza mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH ni Tanzania Communication and Development Centre, Benjamini Mkapa, Amani Girls Home, The Manoff Group na D-Tree International.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabron Masatu akizungumza ofisini kwake kuhusiana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya kuboresha huduma za afya katika Vituo vya Afya na Hospitali ili kukabiliana na vifo vya uzazi kwa akina mama na watoto.
Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabron Masatu akizungumza na timu ya wataalam wa afya mkoani Mara.
Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini, Hellen Magare akieleza namna Serikali ilivyoboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Kisorya kwa kushirikiana na wadau kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisorya, Dkt. Hemedi Hassani akionyesha vifaa tiba mbalimbali kikiwemo kitanda cha upasuaji, mashine ya dawa ya usingizi na mashine ya Oksijeni vilivyonunuliwa katika Kituo cha Afya Kisorya.
Mmoja wa wakazi wa Kisorya wilayani Bunda, Kasenda Kaguba aliyepata huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji katika Kituo cha Afya Kisorya akitoa shukurani kwa Serikali kuboresha huduma za afya katika Kituo hicho.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.