Serikali imesema lango la kuingilia watalii kupitia maeneo ya Kilangali na Tindiga Wilaya ya Kilosa litafungua fursa ya watalii watakaosafiri na treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam na Dodoma kuingia Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa urahisi.
Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mikumi Mhe. Dennis Lazaro Londo, ambaye alitaka kujua Serikali imefika hatua gani katika mchakato wa ujenzi wa Geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga.
Awali Mhe. Kitandula alisema kuwa Serikali imekamilisha tathmini ya awali kwa ajili ya kujenga lango hilo, ambapo gharama za ujenzi wa lango hilo na miundombinu itakayoambatana na lango husika itakuwa Shilingi Bilioni 2.8.
Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa michoro pamoja na BOQ imekamilika. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lango hilo.
Vilevile Mhe. Kitandala aliongeza kuwa Serikali kwa kuona umuhimu wa hifadhi hiyo imejipanga kuongeza malango ya kuingilia watalii katika maeneo yote muhimu ambapo kwa sasa kupitia Mradi wa Kukuza Utalii Kusini (REGROW), malango mawili (2) ya kisasa yanajengwa kwa ajili ya kuingilia watalii katika maeneo ya Doma na Kikwaraza (Mji mdogo wa Mikumi). Ujenzi huo umeanza mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2024.
No comments:
Post a Comment