Habari za Punde

Mkutano wa COP 28 Kuinufaisha Tanzania

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi akiongoza Kikao cha Tatu cha Kamati ya Maandalizi ya mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023. Kikao hicho kimefanyika Dodoma Oktoba 4,2023.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 ni fursa kubwa kwa Tanzania katika ushiriki wake.

Amesema hayo wakati akiongoza Kikao cha Tatu cha Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa COP 28 Dodoma Oktoba 4,2023 akisisitiza kuwa taasisi na sekta mbalimbali lazima ziungane katika hilo.

Mitawi amesema kama nchi lazima kwenda kimkakati ili kuonesha utayari wa kushirikiana na ulimwengu katika mambo mbalimbali na kuonesha fursa zilizopo hapa nchini katika uwekezaji.

“Bado hatujachelewa sababu hii ‘COP’ sio ya mazingira pekee kama wengi wanavyodhani bali inagusa sehemu kubwa katika taifa letu maana hapo ndio sehemu unaweza kupata kampuni kubwakubwa za kuwekeza, unajifunza kutoka kwa wengine vitu vingi kwa wakati mmoja kama vile usafirishaji, utalii, madini na ulinzi,” amesema Mitawi.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi amesema Wizara ya Madini nayo inapaswa kushiriki katika hilo sababu hii ndio nafasi kwao kujifunza kwa wenzao namna wanavyofanya na kupiga hatua katika eneo hilo sambamba na Utalii, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji.

“Kila mtu aone anao wajibu kwenye hili ili kuhakikisha ushiriki wetu unakwenda kuzaa matunda huko tunakokwenda kama taifa lakini kila mmoja akitazama upande wake namna ya kuboresha hapa alipo kwa kujitangaza na kujifunza kwa wenzetu.”

Naye Mhandisi Dorisia Mulashani kutoka Wizara ya Maji amesema watatumia fursa hiyo kuhakikisha wanaboresha zaidi eneo la uwekezaji katika miradi ya maji ili kukuza uchumi kwa kuwepo kwa mabwawa, umwagiliaji endelevu, kuboresha usafi wa mazingira na uwezeshaji wa kijamii.

Mkutano huu unatarajiwa kufanyika katika eneo la Blue Zone (Expo City Dubai) na jumla ya washiriki takriban 100 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kushiriki.

Matarajio ya COP 28 ni pamoja na kuhakikisha msimamo wa Tanzania unakubaliwa, kupata fursa za upatikanaji wa rasilimali fedha kuwezesha utekelezaji wa miradi pamoja na teknolojia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia, nchi inatarajia kuongeza uwekezaji katika Biashara ya Kaboni, kutangaza jitihada za nchi na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi akielezea jambo wakati wa Kikao cha Tatu cha Kamati ya Maandalizi ya mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023. Kikao hicho kimefanyika Dodoma 

Wajumbe wakiwa kwenye Kikao cha Tatu cha Kamati ya Maandalizi ya mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023. Kikao hicho kimefanyika Dodoma Oktoba 4, 2023.


Wajumbe wakiwa kwenye Kikao cha Tatu cha Kamati ya Maandalizi ya mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika Dubai kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023. Kikao hicho kimefanyika Dodoma Oktoba 4, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.