Habari za Punde

Wakulima wa mwani washauriwa kulima kisasa


 Wakulima wa zao la mwani wametakiwa kulima kilimo hicho kisasa ili kukuza mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Hayo yameelezwa na Wakufunzi kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini wakati wakitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima wa zao la mwani juu ya kulima kwa njia bora na kina kirefu cha maji. Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi za Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi zilizopo Maruhubi.
Wakufunzi hao wamesema iwapo wakulima wa zao hilo watalima kwa njia ya maji makubwa mafanikio makubwa watayapata ikiwemo kukuza vipato vyao na kuongeza pato la taifa.
Mkufunzi Pavu Khamisi Mwenyekiti wa Jumuiya za Wakulima wa Mwani amesema mpando wa kamatia chini ni mzuri kwa wakulima wa mwani kulima katika njia hiyo kwani kinakiweka zao hilo salama hata kama maji yakikupwa.
Amesema hivi sasa wakulima wengi wa mwani wanalima kilimo hicho kimazowea hivyo mafunzo hayo yatawasaidia katika kufikia ndoto zao walizo jiwekea katika kukuza vipato vyao.
Nae Joice John Denis ambaye ni Afisa kitengo cha mwani amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuona kinamama na vijana wanapenda kulima kilimo hicho na kupata faida pale watakapo uza ili kujikwamua na maisha yao.
Amesema hivi sasa kilimo cha mwani wengi wao ni wanawake karibu ya asilimia 80 hasa watu wazima hivyo wakati umefika kwa vijana kuwa tayari na kulima zao hilo kwa faida yao.
Kwa upande wao Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi katika kuwapatia mafunzo hayo kwani hivi sasa wakulima wengi wa mwani wanalima kimazowea.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliofanyika ofisini Maruhubi ambayo yameandaliwa na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kupitia Mradi wa AFDP, IFAD .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.