Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa mazingira kutoka mataifa 10 duniani yanayotekeleza Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI) yaliyoanza leo Novemba 6, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (kulia) akifuatilia jambo wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa mazingira kutoka mataifa 10 duniani yanayotekeleza Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI) yaliyoanza leo Novemba 6, 2023 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja tathimini na ufuatiliaji wa miradi kutoka Shirika la Kimataifa la Dunia (IUCN) Dkt. Francis Musau. Katikati ni Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Mazingira (IUCN) Bi. Carole Saint-Laurent.
Mmoja wa washiriki wa warsha
ya wadau wa mazingira kutoka mataifa 10 duniani yanayotekeleza Programu ya
Urejeshaji ya kidunia (TRI) akizungumza jambo wakati wa
warsha hiyo iliyoanza leo Novemba 6, 2023 Jijini Dar es Salaam
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema imeendelea kuweka mikakati na mipango mahsusi ili kuhakikisha inarejesha uoto wa asili katika ardhi takribani hekta milioni 5.2 ifikapo 2030.
Hayo yamesemwa leo Novemba 6, 2023
na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua warsha
ya Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI), kutoka mataifa 10 duniani inayotekeleza
Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai ulimwenguni.
Maganga amesema uchumi wa Tanzania
kwa kiasi kikubwa unategemea maliasili ikiwemo misitu, bahari,maziwa, mito,
ardhi oevu, wanyamapori na ardhi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia ukuaji wa
uchumi na kupunguza umaskini, hata hivyo matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali
hizo yameleta tishio la uwepo wa rasilimali hizo.
“Upotevu wa bioanuai ikiwa ni pamoja na viumbe wengine
wa majini unachochewa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo
endelevu ikiwemo kilimo na matumizi mengine ya ardhi yasiyo endelevu….Tumeanzisha
programu mbalimbali za urejeshaji wa uoto wa asili ikiwemo kampeni ya upandaji
wa miti katika maeneo mbalimbali ya nchi” amesema Maganga.
Kwa mujibu wa Maganga amesema inakadiriwa duniani kote
takribani ekari milioni 18.7 za misitu hupotea kila mwaka na kutokana
na umuhimu wa urejeshaji wa ardhi, Tanzania imetenga ukubwa wa eneo takriban asilimia
40 ya eneo lote la ardhi ikijumuisha 6.5% ya bahari na 33% ya maeneo ya nchi
kavu.
Maganga amesema katika kuunga mkono juhudi za
kidunia za urejeshaji wa ardhi na uhifadhi wa mazingira, Tanzania imezindua sera
mpya ya Taifa ya Mazingira (2022) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (2022-2032) ambao umezingatia mipango shirikishi ya usimamizi wa
mazingira katika ngazi zote.
Alisema lengo la mradi huo
wa TRI ni kuimarisha
usimamizi wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi
wa mifumo-ikolojia na jamii kwa na ni sehemu ya mradi mkubwa wa kidunia
unaotekelezwa katika nchi 11 duniani ikiwemo Tanzania
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa
Rais, Bi. Kemilembe Mutasa amesema warsha hiyo ya siku tano imekusudia kuwakutanisha
wataalamu hao na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa miradi ya
urejeshaji katika mataifa 10 duniani na kuanisha mbinu za upatikanaji wa
rasilimali muhimu za usimamizi wa miradi hiyo.
“Warsha hii imeshirikisha wataalamu wanaotekeleza
mradi wa TRI na kwa pamoja tutajengeana uwezo, mbinu na mikakati mbadala yenye
uhalisia na nadharia ya kila nchi kutoka katika katika ukanda katika namna
inavyotekeleza na kusimamia miradi ya TRI” amesema Kemilembe.
Kwa upande wake Meneja Tathimini na Ufualitiaji wa Shirika
la Kimataifa la Mazingira (IUCN) Tanzania Dkt. Francis Musau ameishukuru Ofisi
ya Makamu wa Rais kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi Wa urejeshaji na kuwa kuitaja
kuwa ni miongoni mwa nchi ya mfano inayotekeleza vyema miradi hiyo ya TRI.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya
Bioanuai (SLR) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda amesema malengo
ya mradi huo ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na urejeshwaji wa
ardhi iliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa
mifumo-ikolojia na jamii nchini.
Amesema mradi huo hapa nchini unatekelezwa
katika katika Mikoa 5 Halamshauri 7, Kata 18 na Vijiji 54 ambapo eneo la mradi
linajumuisha mifumo ikolojia ya mabonde matatu ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa.
Alizitaja Halmashauri
zinazotekeleza mradi huo ni pamoja na Halmashauri za Wilaya za Iringa Vijijini
(Iringa), Mbeya na Mbarali (Mbeya), Wanging’ombe (Njombe), Halmashauri za
Sumbawanga vijijini (Rukwa), Tanganyika, na Mpimbwe (Katavi).
Mradi unafadhiliwa wa SLR
unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF). Nchi nyingine zinazotekeleza
mradi huo ni pamoja na Cameroon, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Guinnea Bissau, Kenya, Myanmar, Pakistan, Sao Tome&
Principe.
MWISHO
No comments:
Post a Comment