Habari za Punde

WASICHANA MIAKA 14 WANATARAJIWA KUPATA CHANJO YA (HPV) DISEMBA 1-2,2023

 
Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt.Salim Slim akitoa taarifa Kwa vyombo vya habari kuhusiana na zoezi la chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi inayoenda kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 katika skuli zote Unguja na Pemba ifikapo Disemba 1-2 mwaka huu.

PICHA  NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO 


Na Fauzia Musa , Maelezo Zanzibar

Mkurugenzi Kinga  na Elimu ya Afya Zanzibar Dk Salim Slim  amewataka Wazazi, walezi na walimu wakuu kushirikiana ili kufanikisha zoezi la utoaji wa  chanjo ya kinga dhidi ya Saratani ya Shingo  ya mlango wa  kizazi kwa wasichana wenye umri  wa miaka 14 katika skuli zote Unguja na Pemba.

Akitoa taarifa kwa  Waandishi wa habari kuhusiana na zoezi hilo huko Ofisini kwake  Mnazimmoja  Mjini Unguja Dkt Salim amesema kukamilika kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza  tatizo hilo Nchini.

Alisema zoezi hilo linatarajiwa kufanyika Disemba 1 na 2 mwaka huu katika Skuli zote Unguja na Pemba na kuwasisitiza walimu na wazazi kuwahimiza wasichana hao kushiriki katika zoezi hilo kutokana na baadhi ya  skuli kufungwa.

Alifahamisha kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imehakikisha chanjo hiyo kuwa ni  salama na haina madhara na imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO ambayo itatolewa katika mikoa yote ya Tanzania   kwa lengo la kukinga Afya za Wasichana . 

 

Dkt. Salim ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ilizindua rasmi chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi  Aprili 19,2018 kwa lengo la kuwakinga wanawake na wasichana dhidi ya ugonjwa huo visiwani  Zanzibar.

 

Chanjo hiyo itasimamiwa na Wizara ya Afya kupitia  Mradi wa MCGL  unatekelezwa na  JAHPIEGO kwa ufadhili wa shirika la Msaada la Marekani USAID.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.