JOPO la majaji ambao ni wataalamu na wajuzi katika fani ya habari wameanza kazi ya kuchambua kwa kina kazi za
Waandishi wa Habari wanaowania Tuzo ya Umahiri katika uandishi wa habari za
takwimu zinazohusu masuala ya Wanawake na Uongozi Zanzibar.
Majaji hao wanatoka katika vyombo mbalimbali vya habari, ikiwa ni
pamoja na magazeti, redio, televisheni, na mitandao ya kijamii.
Uteuzi huu umefanyika kwa kuzingatia sifa za usiri na uadilifu ili
kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa ufanisi.
Majaji hao watafanya kazi kwa siku tano (5) ya kupitia kazi na
kuandika ripoti kamili inayoonesha mchakato pamoja na washindi wa kwanza hadi
watatu kwa kila eneo.
Vigezo vinavyoangaliwa ni pamoja na makala hizo kuzingatia mada husika
lakini pia kuwepo kwa ubunifu wa mada, habari iliyokuwa na vyanzo tofauti vya
habari pamoja na makala au vipindi hivyo kuzingatia masuala ya jinsia na
makundi ya pembezoni.
Tuzo hizo ambazo kauli mbiu yake ni “kalamu yangu, mchango wangu kwa wanawake”, zinalenga kuhamasisha
waandishi wa habari kutumia kalamu na vyombo vya habari kuelimisha umma umuhimu wa nafasi za wanawake
katika uongozi, hivyo kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za
ngazi za maamuzi.
Kalamu za waandishi wa habari hazina budi kulenga katika kuinua
wanawake ili waweze kushiriki katika uongozi ikiwa ni sehemu muhimu ya
kuimarisha usawa na haki kwa wanawake na wanaume kama inavyoeleza katika katiba
ya Zanzibar ya 1984.
Hata hivyo TAMWA, ZNZ inawashukuru Waandishi wa Habari Zanzibar kwa
kuonesha mwitikio wa kuandika habari za takwimu kuhusu wanawake na uongozi,
ambapo kumekua na ongezeko la kazi mwaka huu ambazo ni 529 ukilinganisha na
mwaka jana ambapo waandaaji walipokea kazi 421.
Aidha TAMWA ZNZ inatoa wito kwa Waandishi wa Habari kuendelea kutumia
kalamu zao kuandika makala na kuandaa vipindi kuhusu takwimu za wanawake na
uongozi, huku wakisisisitiza umuhimu wa kuinua wanawake katika kushika nafasi
mbalimbali za uongozi.
Tuzo hizi zinatolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa
kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL). Mradi huo unatekelezwa
na TAMWA Zanzibar, Jumuia ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), pamoja na
Jumuia inayojihusisha na Mazingira, Usawa wa Kijinsia, na Utetezi Pemba
(PEGAO), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania.
Imetolewa na kitengo cha habari,
TAMWA ZNZ.
No comments:
Post a Comment