Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh Rachel Kassanda ( Kulia ) akizindua programu jumuishi ya Taifa ya malezi , makuzi na maendeleo ya mtoto ( PJT-MMMAM) katika ofisi ya mkuu wa Wilaya Alhamisi Febuari 15, 2024, (kushoto ) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi. Fidelica Myovella.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda akikabidhi programu jumuishi ya Taifa ya malezi , makuzi na maendeleo ya mtoto kwa mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu baada ya kuzindua programu hiyo .
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Rachel Kassanda akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa hafla ya Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi na Maendeleo ya Mtoto.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Rachel Kassanda akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu jumuishi ya Taifa ya malezi , makuzi na maendeleo ya mtoto ( PJT-MMMAM) katika ofisi ya mkuu wa Wilaya leo Alhamisi Febuari 15, 2024.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Rachel Kassanda amezindua programu ya malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT MMMAM) katika Halmashauli ya Wilaya ya Magu ikiwa na lengo la kukabiliana na kutokomeza changamoto zinazoonekana kuwa ni kikwazo cha hatua sahihi za ukuaji timilifu wa mtoto kimwili, kiakili na kijamii.
Akizungumza wakati akizindua programu hiyo leo DC Kassanda ametoa rai kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu na idara zote zinazotekeleza program hii kwa kushirikiana na wadau kuzingatia utekelezaji Programu hii kwenye maeneo yao kupitia maelekezo na ushauri utakaokuwa na unaotolewa mara kwa mara.
Amesema Uzinduzi huu unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuwa Programu hii izinduliwe ngazi zote kuanzia Taifa, Mkoa hadi Halmashauri.
"Uzinduzi huu uambatane na utekelezaji wake kwa kuweka Mipango Kazi na kusaidia utengaji wa bajeti na kutoa fedha kwa utekelezaji; amesema "
Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Magu, Coretha Sanga amesema kuwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM), inayotekelezwa kuanzia 2021/22 hadi 2025/26, inakusudia kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto.
Ameongeza kuwa Programu za malezi jumuishi nchini Tanzania zinahitaji kupewa kipaumbele na msisitizo, kutokana na kukosekana kwa uratibu mzuri.
"Mara nyingi zinatekelezwa kama sehemu za programu za kisekta au tafiti zinazofanywa na wadau zikilenga baadhi ya umri wa watoto na kutekelezwa kwenye maeneo machache"
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi. Fidelica Myovella amesema Halmashauri imejipanga kutekeleza programu hiyo kwa kushirikiana na wataalamu na wadau na kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na Mkuu wa Wilaya ili kufikia malengo ya utekelezaji wa programu hiyo.
uzinduzi Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika Wilaya ya Magu imezinduliwa leo Febuari 15 ikiwa ni muendelezo baada ya uzinduzi ngazi ya Mkoa tarehe 22/9/2023 na ngazi ya Taifa Disemba, 2021.
No comments:
Post a Comment