Habari za Punde

Uzinduzi wa Ukataji wa Bima ya Vyombo vya Moto Kupitia Kampuni ya Simu ya TigoZantel

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Saada Mkuya Salum, amesema uzinduzi wa upatikanaji wa bima ya vyombo vya moto kwa njia ya mtandao ni njia bora ya wananchi kupata bima kupitia njia ya simu kwa urahisi.
Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya uzinduzi wa mashirikiano kati kampuni ya simu ya Tigo Zantel na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.

Alisema hayo ni mapinduzi makubwa katika huduma za utoaji wa bima hapa Zanzibar ambayo yanakwenda kutoa suluhisho na changamoto kwa mji wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambao umekuwa sana.

Aliipongeza tigo Zantel na ZIC kwa ubunifu huo ambao unakwenda kutatua changamoto katika upatikanaji wa huduma kwa urahisi.   

Waziri Saada alibainisha kuwa hatua hiyo pia itasaidia kuondoa msongamano katika kituo kinachotoa huduma za hizo na mwananchi kupata kupitia simu yake ya mkononi.

Alisema Zanzibar inaendelea kutafuta njia za kutoa katika huduma za kutumia makaratasi na kutumia mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuendesha uchumi wa Zanzibar. 

Hata hivyo alifahamisha kuwa mashirikiano hayo kati ya Tigo Pesa na ZIC inapelekea serikali kufikia malengo yake ya kuwa na uchumi usio wa fedha taslim.

“Mmekwenda haraka zaidi kuliko vile ambavyo tumepanga hivyo angalieni ubunifu mwengine ambao utatuwezesha sisi kufikia malengo yetu kwa haraka zaidi,” alisisitiza.

Alisema bado wananchi hawajaona umuhimu wa kuwa na bima hivyo aliwaomba kuendelea kutoa elimu huku serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa sera na sheria ili kuona sekta binafsi na sekta za umma zinasaidia maendeleo ya nchi yao. 

“Ni lazima mapinduzi haya yaendane na namna bora ambayo itawafanya watu kuwa na bima kwani asilimia tano bado ni ndogo nasi serikali tupo tayari kuona sekta zote zinashirikiana pamoja katika utoaji wa huduma,” alisema.

Mbali na hayo alisema anaamini mashirikiano hayo yataleta tija zaidi kwa wananchi wote wanaotumia huduma za Shirika la Bima Zanzibar.

Naye, Ofisa Mkuu Tigo Pesa, Angelica Pesha, alisema ushirikiano wao wa kimkakati kati ya Tigo Pesa na ZIC kwa kuitambulisha huduma mpya ya bima ya vyombo vya moto ya kidijitali kwani hivi sasa dunia inakwenda huko.

Alisema ushirikiano wao kati ya Tigo na ZIC ni hatua nyengine muhimu katika kuendeleza falsafa yao ya kuhakikisha watanzania wote wanajumuishwa katika huduma za kifedha na za kidijitali.

Ofisa huyo alisema kupitia bima ya vyombo vya moto ya Tigo Zantel itawawezesha wateja wa Tigo Pesa kutoka Tanzania bara na visiwani kununua bima kwa vyombo vyao kupitia simu zao za mkononi.

Alifahamisha kuwa huduma hiyo ya kibunifu imejumuisha aina mbalimbali za vyombo vya moto ikiwemo vyombo binafsi na vyombo vya biashara ili kuwarahisishia wateja kupata bima kwa urahisi.

Hata hivyo, alisema asilimia 10 tu ya watanzania ndio wanaotumia huduma za bima kama ilivyoainishwa na ripoti ya fedha ya mwaka 2023 hivyo ni jukumu lao kama watoa huduma kuongeza ubunifu na kuondoa changamoto zinazokwamisha watanzania kutumia huduma za bima.

Aliahidi kuwa Tigo Pesa ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa huduma za kifedha kuhakikisha watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma za kifedha ikiwemo huduma za bima.

Mbali na hayo, alisema kupitia ushirikiano huo wa kipekee na ZIC wanaamini wataendelea kupunguza pengo lilokuwepo kuhakikisha huduma za bima zinapatikana kirahisi na uharaka zaidi na kupunguza gharama za wateja kufikia huduma hizo, hivyo aliwataka wateja wa tigo Zantel kuchangamkia huduma hizo ili kulinda vyombo vyao vya moto.     

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Arafat Haji, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kuunganisha uwezo wa teknologia na huduma bora ya bima kutoka shirika hilo ili kuwapata wateja urahisi na kupata huduma popote walipo.

Alisema sekta ya teknologia imekuwa muhimu pamoja na ukuaji katika sekta ya bima ambayo inabadilika kwa kasi kila siku.

Mkurugenzi Arafat alisema ushirikiano wao na Tigo Pesa unakwenda sambamba na dhamira yao ya kuwa mstari wa mbele katika ufikiwaji wa huduma za bima na kuongeza ubunifu na mageuzi.

Kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na Tigo Pesa tumeunda suluhisho hili sio tu la kuaminika lakini urahisi wa ufikiwaji kuliko hapo awali,” alisema.

Alisema ushirikiano huo pia ni muendelezo wa jitihada zao za kukidhi mahitaji ya wateja wao ambayo yanabadilika kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali na ushirikiano wao unakwenda kufungua njia mpya na kuchochea ubunifu katika utoaji wa huduma zao kwa wananchi.


Mkurugenzi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Arafat Haji, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kuunganisha uwezo wa teknologia na huduma bora ya bima kutoka shirika hilo ili kuwapata wateja urahisi na kupata huduma popote walipo.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.