Habari za Punde

WAZIRI JAFO AFUNGUA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewapongeza watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kufanya kazi kwa bidii na kudumisha Muungano.

Amewapongeza watendaji hao kwa kujituma katika kuwezesha kufanyika kwa vikao vya Masuala ya Muungano ambavyo vina kazi ya kujadili masuala ya Muungano.

Akifungua Mkutano wa Nne wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Machi 26, 2024 jijini Dodoma, Dkt. Jafo amesema mafanikio ya utekelezaji wa majukumu hayo ni matunda ya ushirikiano baina ya watumishi katika Ofisi hiyo.

Amesema katika kuelekea miaka 60 ya Muungano yapo mengi ya kujivunia yakiwemo utatuzo wa chanamoto za Muungano kutokana na maelekezo ya viongozi wa kitaifa, ambayo kwa kiasi kikubwa ni matunda ya utendaji wa watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais

Pia, Waziri Jafo amewapongeza watendaji hao kwa kusimamia vyema miradi ya mazingira ambayo imewajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sanjari na hilo amewaasa kuendelea kushikamana na kufanya kazi kwa kujituma ili mafanikio makubwa yanayopatikana kupitia miradi hiyo yaendelee kuwanufaisha wananchi.

Amesema kuwa kila mmoja ana mchango katika mafanikio yanayopatikana katika Ofisi na kwamba anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii na taifa kwa ujumla hivyo anapaswa kuacha alama.

“Mnakumbuka katika moja vikao vya wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais niliwahi kusema kwamba kufanya kazi ni moja ya ibada, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuitendea haki nafasi aliyonayo ili mchango wake uendelee kuwa mfano wa kuigwa na matokeo ya Ofisi hii yaendelee kuwa mfano wa kuigwa,” amesema.

Kadhalika, Dkt. Jafo amesisitiza jukumu lililopo mbele ni kuhakikisha maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Sukuhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za afya na mazingira yanafikiwa.

Kwa upande mwingine amewapongeza wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais walioshiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 ambao ulikuwa na kaulimbiu ‚Tunza Mazingira Okoa vyanzo vya Maji, kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa” kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

Amesema elimu ya mazingira inayotolewa imesaidia kukuza uelewa wananchi katika zoezi la upandaji wa miti hususan katika kila halmashauri ambapo katika kipindi cha mwaka huu tayari miti zaidi ya milioni 270 imeshapandwa katika halmashauri zote nchi.

“Ni matumaini yangu kuwa ushiriki wetu mwaka huu utakuwa umeboreshwa zaidi ili kupata muda wa kutosha kukutana na wananchi na kutoa elimu ya mazingira kwa umma wa watanzania wenzetu kote nchini,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bi. Mary Maganga amesema ushirikiano baina ya wafanyakazi, upendo na kujituma katika kazi itasaidia kuleta matunda mazuri.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Bw. Jonas Rwegoshora ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais namna watumishi wake wanavyofanya kazi kwa ushirikiano.

Amesema huo ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine ambazo katika mikutano kumekuwa na migogoro tofauti alivyoshuhudia kwenye mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.