RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa
shukrani zake za dhati kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa
kuendelea kumuombea du’a na khitma baba yake Mzazi Hayati Mzee Ali Hassan
Mwinyi aliefariki hivi karibuni.
Al hajj Dk. Mwinyi, ametoa shukurani hizo mara baada ya ibada
ya sala ya Ijumaa iliyofuatiwa na visomo mbalimbali, hitma na du’a kweye masjid
Hidaya, Kilimani Tazari, Mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Familia yake, Al hajj Dk. Mwinyi amewashukuru
wananchi hao kwa mapenzi yao kwa Mzee Mwinyi tangu walipomuuguza hadi alipokufa
Februari 29 mwaka huu.
Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Rashid Hadid Rashid alisema wanachi
wa Kijiji cha Kilimani Tazari na vijiji
jirani, kwa makusudi waliamua kukaa
pamoja kumuombea du’a Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, viongozi waliopo hai na
wazee wa vijiji hivyo waliofariki dunia.
Akizungumza kwenye ibada hiyo, Sheikh Khamis Abdul Hamid
aliwahusia waumini wa kiislam kuendelea kufanya mema na kumcha Mwenyezi Mungu
kwa haki ili roho zao zikawekwe mahala pema baada ya kufa.
Mapema akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa, Khatib Sheikh, Omar
Abdi aliwasihi wananchi na waumini wa dini ya Kiislam kuendelea kujenga hofu
kwa Mwenyezi Mungu kwa kukithirisha ibada hata baada ya kumalizika kwa Mwezi
mtukufu wa Ramadhan.
Aliusia kwamba
Mwenyezi Mungu hayupo Mwezi wa Ramadhan pekee bali yupo siku zote, hivyo
aliwanasihi waumini hao, kuendeleza ibada kwa siku za kawaida kama ilivyokuwa
Ramadhan.
Ibada hizo za visomo
na du’a na hitma pia waliombewa viongozi waliopo serikalini, wastaafu, masheikh
na wazee walio hai na waliotangulia mbele ya haki ndani na nje ya Mkoa huo.
Hafla hiyo pia
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwemo Mufti Mkuu wa
Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kaab, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid
Hadid na viongozi wengine.
IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment