Habari za Punde

KINANA: SERIKALI YA RAIS SAMIA ITACHUKUA HATUA KUKABILI ATHARI ZA MVUA.

 

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza na Viongozi  wa CCM katika kikao maalum Cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara katika Ziara ya Kuimarisha Chama Mkoani humo.

Viongozi na Wanachama Mbalimbali wakifuatilia  kikao maalum Cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Mjini kilichohudhuliwa na makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Ndg. Abdulrahman Kinana.

Na Mwandishi Wetu Musoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Abdulrahman Kinana amesema Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla inafuatilia kwa makini uharibifu mkubwa wa miundombinu unaosababishwa na mvua zinazoendelea kunyeesha nchini.

Amesema kuwa katika maeneo ambayo yameathirika sana, Serikali imepeleka fedha kukarabati miundombinu hiyo na misaada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wahanga.  

Kinana ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini ambao walieleza uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla kutokana na mvua zinazoendelea kunyeesha.

"Serikali inaendelea kufanya tathmini ya uharibifu huo wa miundombinu ili kutenga fedha za kukarabati maeneo yote ambayo yameathirika.Uharibifu wa miundombinu umefanyika katika nchi mbalimbali duniani hata zile zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo na sio Tanzania peke yake. 

"Kwa mara ya kwanza tumeona duniani nchi nyingi zimepatwa na mafuriko, hata zile ambazo katika historia hatukuwahi kuona mvua, hivyo sio sisi peke yetu, haya yote yametokana na mabadiliko ya tabianchi, mahitaji ya kufanya marekebisho ni makubwa na yataendelea.

"Niwaambie Rais Samia anapata taarifa kuhusu haya yanayotokea katika mikoa mingi, sehemu ambapo miundombinu imeharibika sana hadi kukosekana kwa mawasiliano hatua za dhati zimechukuliwa," alisema.

Makamu Mwenyekiti Kinana alieleza kuwa, kutokana na changamoto hiyo wananchi wengi wanahitaji miundombinu iliyoharibika katika maeneo yao ikarabatiwe na kwamba, Rais Dk. Samia anapata taarifa kila siku kuhusu matukio yanayotokana na mvua hizo.

"Sehemu zingine tunawaomba watanzania wawe wavumilivu kusubiri mvua ziishe ili ukarabati utakapofanyika uwe wa uhakika. Pia itatoa nafasi kwa serikali kujipanga vizuri ukarabati utakapoanza ufanyike sehemu kubwa nchini," alisema.

Katika hatua nyingine, Kinana alisema kuwa CCM itajadili kwa kina suala la kikokotoo kutokana na kuongezeka kwa malalamiko nchi nzima.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mwalimu Silanga wa Shule ya Msingi, Wilaya ya Musoma Vijijini Nyakusanya Mkangara aliyetaka Chama kiishauri Serikali ilegeze msimamo wake kwakuwa kikokotoo si rafiki, kitawaumiza wastaafu.

"Malalamiko yapo na yanaendelea kuongezeka lazima tuwe na majibu sahihi ya jambo hilo na mimi nalichukua ndugu Mwenyekiti wa Walimu naenda kushirikiana na wenzangu kulijadili vizuri kuona njia nzuri, inayofaa," alieleza Kinana.

Wakati huohuo Makamu Mwenyekiti Kinana alimsifu Rais Dk. Samia kwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo kwa Watanzania ikiwamo kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali bila ya wananchi kushurutishwa au kuporwa fedha zao.

"Kwa nini tusitoe pongezi kwa Rais Samia?. Amefanya kazi nzuri, anajitoa, anajituma na kubwa amekuwa kiongozi wa mfano anaongoza nchi yetu vizuri na maendeleo yanapatikana kila mahali na Musoma hapa ni mashahidi.

"Hata katika ukusanyaji wa mapato hakuna mwaka tumepata mapato makubwa bila kufunga watu, bila kupora watu. Huu ndio ukweli, Watanzania tumuunge mkono.

"Musoma hapo nyuma nikiwa Katibu Mkuu nilikuja kufanya ziara kulikuwa hakuna maendeleo kama ilivyo sasa. Mbunge wa Musoma Mjini (Vedastus Matayo) ameeleza kuwa Musoma hamna shida ya barabara za lami, maana zipo.

"Shule ziko nyingi, maji yapo ya kutosha, hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inaendelea vizuri, Rais amefanya mambo makubwa ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.