Habari za Punde

Wizara ya Fedha Yaanza Kutekeleza Mkakati wa Kutoa Elimu ya Fedha

Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali na wananchi wa kata ya manyoni, wilayani Manyoni mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha kutoa elimu ya fedha vijijini ili kuwapa uelewa wajasiriamali na wananchi kuwa na matumizi sahihi ya fedha na kuepukana na madhara ya mikopo umiza.
Baadhi ya wajasiriamali na Wananchi wa Kata ya Manyoni, wilayani Manyoni Mkoani Singida wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu matumizi ya fedha binafsi, umuhimu wa kuweka akiba, pamoja na mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa, na utunzaji wa fedha binafsi. 
Mmoja wa wajasiriamali waliyoshiriki katika mafunzo ya elimu ya fedha, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha katika Kata ya Manyoni, wilayani Manyoni mkoani Singida Bi. Luciana Eliya (aliyesimama), akieleza namna alivyofaidika na elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha.

Na. Asia Singano, WF, Singida 

Wizara ya Fedha imeanza kutekeleza mpango wake wa kutoa elimu ya fedha vijijini awamu ya kwanza kwa baadhi ya mikoa ikiwemo Mkoa wa Singida ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kifedha ikiwemo kukabiliana na mikopo umiza, matumizi bora ya fedha na utunzaji wa fedha binafsi na kuweka akiba.                      
           
Hayo yameelezwa na Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, Wilayani Manyoni mkoani Singida wakati  akitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.

Bw. Kimaro alisema kuwa ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi wengi kumesababisha baadhi ya wananchi kupoteza mali zao kutokana na kukopa sehemu mbalimbali huku wakishindwa kurejesha kutokana na riba kuwa kubwa na kutumia fedha hizo bila kuzalisha faida.

‘’Kumekuwa na changamoto nyingi, wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha na hivyo kusababisha kupata changamoto nyingi ikiwemo kuomba mikopo kupitia taasisi zisizo rasmi ambazo wanaposhindwa kulipa mikopo husika taasisi hizo hutaifisha mali zao’’ alisema Bw. Kimaro.

Aliongeza kuwa katika kutatua changamoto za mikopo ya “kaushadamu”, Wizara ya Fedha inalenga kuelimisha wananchi wote juu ya mambo ya kuzingatia kabla ya kuomba mkopo, ikiwemo kukopa kwa malengo maalumu, na kutekeleza lengo husika baada ya kupata mkopo katika taasisi za huduma za fedha zilizosajiliwa.

Kwa upande wake, Bw. David Julius, ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, alikiri kuwa ni miongoni mwa waathirika wa mikopo umiza na kumsababishia hasara zilizotokana na ukosefu wa elimu ya fedha.

Bi. Priscadian Maleta naye ni moja ya wajasiriamali waliyoshiriki na kupata elimu hiyo ya fedha ambaye alisema kuwa, kwa sasa kutokana na mafunzo hayo wananchi wengi wa Manyoni wataepukana na mikopo umiza kwakuwa tayari wamepata elinu ya fedha.

‘’Kutokana na hii elimu niliyoipata leo kwa maana hiyo imenisaidia si mimi tu imetusaidia wajasiriamali wote tulioshiriki, tukipata pesa tutaitumia utaenda kutumia sawa sawa na yale malengo ambayo tumepanga’’ alisema Bi. Priscadian.

Hata hivyo Wizara ya Fedha ilianza kutoa elimu ya fedha kwa baadhi ya maeneo ya mjini ambapo kwa sasa imedhamiria kutoa elimu hiyo vijijini huku awamu hii ikianza katka wilzya mbalimbali za mikoa wa Singida, Manyara na Kagera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.