Habari za Punde

MAJALIWA: TUTAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UVUVI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimsikiliza Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani (kuli) aliyepewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Chato Kati mkoani Geita, Juni 3, 2024. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye uwanja wa Chato Kati akiwa katika ziara ya kikazi ya Mkoa wa Geita, Juni 3, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uvuvi katika maeneo mbalimbali kwa kujenga miradi ya masoko ya samaki yatakayowawezesha wananchi kufanya biashara zao kwa ufanisi na kukuza uchumi.

Amesema hayo leo (Jumatatu, Juni 03, 2024) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mwalo wa kupokelea samaki na soko la kisasa la samaki Chato Beach akiwa katika ziara ya siku moja wilayani Chato, Geita. Amesisitiza kuwa Serikali  imetahakikisha inaimarisha na kuwashirikisha wavuvi na wafugaji katika mipango ya maendeleo yao.

 

Amesema kuwa mradi huo unaotoa fursa kwa yeyote aliyeanza na anayetaka kujikita kwenye sekta ya uvuvi kunufaika na kujiongezea kipato. “Kitendo cha Serikali kuleta soko hili hapa ni kuhakikisha wanasogeza fursa kwa wavuvi  wa eneo hili, soko hili ni lenu, imarisheni uchumi wenu kupitia soko hili.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuidhhinia fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Chato zikiwemo shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya shughuli za uvuvi.


Awali, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi George Kwandu alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza upotevu wa samaki hususan dagaa baada ya kuvunwa, pia utaongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti 2, 2024.


Aliongeza kuwa soko hilo litakuza biashhara ya samaki na mazao yake na kuongeza uhakika wa chakula na lishe. “Soko hili linakwenda kutoa ajira 1,473 kwa wadau mbalimbali wakiwemo wavuvi, wafanyabiashara, wachuuzi, mama na baba lishe na hivyo kukuza kipato cha wananchi na kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za uvuvi.”


Meneja huyo alisema mradi huo wenye gharama ya shilingi bilioni 1.75 unajumuisha miundombinu mbalimbali likiwemo soko la kisasa la kuuzia samaki jumla na rejareja, jengo lenye mtambo wa kukaushia dagaa (tani 10 kwa siku), jengo la mtambo wa kuzalisha barafu na vyumba vya ubaridi kwa ajili kuhifadhia samaki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.