Habari za Punde

WANAOFANYA VITENDO VYA ULAWITI, KUCHUKULIWA HATUA KALI .

Na Hamida Kamchalla, PANGANI.

MKUU wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala ameanza kuvalia njuga vitendo vya ubakaji na ulawiti huku akiliagiza jeshi la polisi wilayani humo kumfuatilia na kumkamata mtu mmoja katika kijiji cha Bushiri ambaye ameripotiwa kwa tuhuma za kuwashawishi watoto wa kiume ili afanye nao vitendo hivyo. 

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku uuzwaji wa pombe majumbani ambao umebainika kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa familia hususani wakati ambao watu wanaanza kulewa.

Kilakala alitoa maagizo hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ccm Wilaya ya Pangani kwa kipindi cha miezi 6 huku akiitaka jamii kuungana kuhakikisha wanafanikiwa kwenye vita dhidi ya ukatili huo kwa watoto. 

Mkuu huyo wa Wilaya alitolea mfano mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu kwenye kijiji hicho ambaye mara kadhaa mtu huyo amekuwa akimrubuni kwa kutaka kumlawiti na kwamba ameripoti maeneo kadhaa lakini mtu huyo bado hajachukuliwa hatua. 

"Nilikwenda kwenye shule moja (jina lake limehifadhiwa) hapa Bushiri mtoto mmoja akizungumza kwa uchungu kabisa kwamba kuna mtu anamtaka kimapenzi,  tungekuwa na watoto majasiri kama yule hili tatizo lingekwisha kabisa,

"Alishika maiki akanambia, 'mkuu wa wilaya mimi binafsi nimefanyiwa ukatili wa kijinsia kuna mzee ananitaka mimi kimapenzi hali yakuwa anajua mimi ni mtoto wa kiume, "alisema DC Kilakala

"Nimempongeza yule kijana kwa kuwa jasiri, watoto wetu mpaka wanaharibika ndio tuchukue hatua nimeliagiza jeshi la polisi yule mzee anayetuhumiwa wamuhoji atuambie kazi zile anazifanya na nani na ameshawaharibu watoto wangapi Bushiri"alisema Kilakala. 

Kuhusu uuzaji wa pombe majumbani Kilakala alisema baadhi ya kaya zinazouza pombe watu wanapoanza kulewa wanawabaka watoto wa familia bila mama mzazi au baba mzazi kujua kutokana na kuwa bize na biashara hiyo. 

Kufuatia hali hiyo Kilakala amepiga marufuku pombe kuuzwa majumbani na tayari wameshaanza kuyafungia baadhi ya maeneo ambayo walevi hufanya vitendo vya hovyo eneo ambalo wanafunzi wanapita wakitoka mashuleni wa wengine kwenda kuiga na kupelekea mmomonyoko wa maadili. 

"Nimemuelekeza ofisa biashara kupitia Mkurugenzi maeneo yote yanayoendesha biashara kiholela yafungiwe mpaka hapo yatakapopata leseni lakini tumemwelekeza Mkurugenzi watoto hakuna kurudi shule usiku, watoto wanarudi nyumbani saa mbili usiku mpaka saa nne usiku,

"Nielekeze kuwa, muda wa masomo uzingatiwe na watoto warudi muda waliopangiwa na mzazi ukiona mtoto hajarudi mpaka saa kumi uanze kuwa na wasiwasi sio mtoto anarudi saa nne usiku unasema hiyo kawaida yake" alisisitiza Kilakala. 

Awali akizungumzia mafanikio waliyoyapata katika Wilaya hiyo Kilakala alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewafanyia maendeleo makubwa ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.