Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameondoka Zanzibar na ujumbe wake kuelekea Shanghai, China, kushiriki katika Maonyesho ya 7 ya China International Import Expo (CIIE), yatakayofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 10 Novemba 2024.

Maonyesho hayo, yenye kaulimbiu “Enzi Mpya, Mustakabali wa Pamoja,” yanajumuisha Maonyesho ya Biashara na Kongamano la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao. 

Tanzania imepewa heshima maalum kuwakilisha bara la Afrika kutokana na mchango  mkubwa wa zaidi ya Kampuni 17 pamoja na sekta za kilimo, kazi za sanaa za mikono, bidhaa za kilimo na uchumi wa buluu.
Ushiriki wa Rais Dk. Mwinyi katika maonyesho hayo unatokana na mwaliko rasmi kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania.

Kabla ya kuelekea Shanghai, China, Rais Dk. Mwinyi na ujumbe wake anatarajiwa kuwasili Doha, Qatar, ambapo atapokelewa na Naibu Mkuu wa Itifaki wa Qatar, Youssef Al Harami, kwa niaba ya Amiri wa Taifa la Qatar, Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani, na kutembelea soko la kihistoria la Souq Waqif.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.