Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Londo Awapongeza Wadau wa Maendeleo kwa Kusaidia Jitihada za Serikali

Na. Mwandisi Wetu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewapongeza wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuongeza nguvu katika jitihada za Serikali za kutoa huduma bora ya afya nchini.

Pongezi hizo zimetolewa wakati Mhe. Londo alipotoa salamu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Jukwaa la Wauzaji na Wanunuzi wa Dawa za Kufubaza Virusi vya UKIMWI tarehe 18 Novemba, 2024 jijini Dar es Salaam, kufunguliwa na Naibu Waziri wa Wizara ya  Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel.

Akitoa salamu hizo Mhe. Londo amewapongeza Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania pamoja na wadau wa afya kwa kufanikisha kuandaa jukwaa hilo muhimu ambalo limehudhuriwa na wadau kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo nchi za Afrika.

‘’Tunawashukuru kwa jukwaa hili linalojadili ajenda ya afya ambayo inagusa uhai wa watu wetu, hivyo ni matumaini yangu majadiliano ya jukwaa hili yatakuwa na matokeo mazuri kwa ustawi wa sekta ya afya’’, alisema Mhe. Londo.

Aidha, alieleza kuwa Serikali ipo tayari kusikiliza ushauri, maoni na mikakati itakayotolewa na itatafuta ufumbuzi wa changamoto za huduma za afya kwa kushirikiana na wataalam hao wa afya.

Vilevile, ameeleza suala la afya ni moja ya kipaumbele cha ukanda wa Afrika Mashariki na kwamba jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdau muhimu katika suala la utoaji wa huduma bora za afya ili kuwekeza katika nguvu kazi imara na kuwezesha shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara, uwekezaji na kilimo.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel katika salamu zake ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la maendeleo la USAID kwa jitihada za kusaidia kutokomeza Malaria, UKIMWI na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Aidha, amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Michael Battle kwa uwakilishi wake unaoendelea kuacha alama nchini kwa kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika huduma za afya.

Pia, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya ununuzi na ukaguzi ili kuboresha huduma za dawa na afya kwa ujumla.

‘’ Ni matumaini yangu kuwa kupitia mkutano huu mfumo wa manunuzi utaimarishwa na kuwezesha upatikanaji wa dawa kwa wananchi kwa gharama nafuu’’, alisisitiza Mhe. Mollel.

Kadhalika, akaeleza kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa Tanzania inawekeza katika viwanda vya dawa, sambamba na kujenga uwezo kwenye maeneo ya teknolojia na wataalamu wa afya. Hivyo, akawakaribisha wadau wa afya kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya dawa na vifaa tiba.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Hassan Khamis Hafidhi na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.