RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali za SMZ na SMT, zimeandaa mpango wa kuongeza vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia wenye thamani ya Euro milioni 59.
Amesema, kupitia mpango huo, Serikali hizo zimedhamiria kuviongezea uwezo
vituo vya Ocean Road, Dar es Salaam, Bugando, Mwanza na kuanzisha vituo vipya
vinne kwa hospitali za Benjamini Mkapa Dodoma, KCMC Moshi, Mnazi Mmoja Zanzibar
na Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo kwa
niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan,
alipofungua Ofisi na Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomu
Tanzania (TAEC) kwa Zanzibar, huko
Dunga Zuze, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, kukamilika kwa mpango huo kutaongeza huduma za matibabu ya saratani kwa
kutumia teknolojia ya nyuklia na Tanzania itakuwa na vituo sita vya Serikali
katika kanda zote muhimu nchini.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza ujenzi wa Ofisi na Maabara hiyo ni chachu
ya kuanza kwa ujenzi wa banki kwa ajili ya kuwekea vifaa vya nyuklia kwa hospitali
za Benjamini Mkapa Dodoma na KCMC Moshi.
Amebainisha kuwa teknolojia ya nyuklia
inaweza kutumika katika uzalishaji wa nishati safi ya umeme na kuwa chaguo la
kuvutia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi hasa kwa maeneo yenye
mahitaji makubwa ya umeme na yenye uwezo mdogo wa kutumia vyanzo vingine vya
nishati mbadala.
Ameeleza kwa mendeleo ya
kiteknolojia ya nishati ya nyuklia pia yana uwezo wa kuchukua nafasi muhimu
katika mchakato wa kuhama kuelekea mfumo wa nishati usio na kaboni (Carbon) au
hewa ukaa yanayoweza kuzalisha umeme unaohitajika.
Akizungumzia juu ya
kupunguza athari za mazingira zinazohusiana na uzalishaji wa umeme unaotegemea
vyanzo vyenye mchango mkubwa wa hewa hatari ya kaboni, Rais Dk. Mwinyi amesema ni
jambo la faraja kuona Tanzania imejaaliwa kuwa na utajiri wa madini ya urani
(uranium), ambayo ndio yanayotumika kuzalisha umeme wa nyuklia.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi
amezisisitiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana pamoja na
Wizara ya Nishati na wadau wengine kuandaa mpango thabiti ili kuhakikisha
Tanzania inaanza kunufaika na umeme wa nyuklia.
Amesema lengo la
ufunguzi wa ofisi hizo nchini ni kuongeza usimamiaji na uendelezaji wa matumizi
salama ya teknolojia ya nyuklia kwa wananchi.
Dk. Mwinyi ameeleza
ujenzi wa miundombinu ya ofisi za (TAEC)
nchini itaimarisha uthibiti wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia,
sambamba na kuimarisha utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia ya
nyuklia katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Pia Dk. Mwinyi
ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujenzi wa Ofisi
hiyo kwa Zanzibar pamoja na Kuishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa
ushirikiano hasa kwa kutoa eneo la ujenzi wa ofisi hiyo, na kuweka miundombinu
wezeshi ikiwemo barabara, umeme na maji.
Katika hatua nyengine
Rais Dk. Mwinyi ameeleza sehemu kubwa ya matumizi ya teknolojia ya nyuklia yapo
sekta ya Afya hususan kwenye uchunguzi na matibabu ya saratani, kwa vituo vya
Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Aga Khan, Kituo cha Tiba cha Bugando, Hospitali
ya Besta na Hospitali ya Good Samaritan ni wanufaika wakubwa wa teknolojia
hiyo.
Hata hivyo, Rais Dk.
Mwinyi ameipongeza (TAEC) kwa kukamilisha mradi wa Maabara Kubwa (Maabara
changamano ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia) awamu ya pili jijini Arusha na
kuongeza kuwa maabara hiyo itaongoza kwa Ukubwa kwa ukanda mzima wa Afrika
Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Elimu
Sayansi na Teknolojia, Omar Juma Kipanga amesema, Wizara inaendeleza kuwekeza
kwenye miundombinu na vifaa vya kisasa vya teknolojia ya Nyuklia, kwa lengo la
kuimarisha matumizi na usimamizi sahihi wa mifumo ya nyuklia kwa maendeleo
endelevu ya nchi na ustawi wa jamii.
Aidha, amesema Wizara
inaendelea na mpango wa kuzalisha wataalamu kupitia mpango wa “Samia scholarship
Extended” unaotoa fursa zaidi kwa vijana wa Tanzania kila mwaka kusoma katika
vyuo bora duniani kwa masuala ya Nyuklia.
Amesema (TAEC) kwa
kushirikiana na taasisi ya Nelson Mandela ya Arusha, wameandaa shahada ya juu ya
Elimu ya nyuklia katika dhamira ya kuziba pengo la uhaba wa wataalamu nchini
ambapo hadi sasa nchi nzima wapo wataalamu tisa tu, aidha, kwa kushirikiana na
Chuo Cha Ufundi Arusha wameandaa mafunzo ya ngazi ya Stashahada za fani hiyo,
lengo ni kuona mchango wa masuala ya nyuklia ni mkubwa katika kuimarisha uchumi
na maendeleo ya nchi.
Naye, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui amesema ujenzi wa
ofisi na maabara hiyo hapa nchini, unaakisi dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya kujenga hospitali za Rufaa za Binguni na Mnazi Mmoja zitakazokuwa
na matumizi makubwa ya mionzi hasa kwa Mashine za MRI, X - Ray na City Scan na
kuihakikishaia (TAEC) kufabya kazi bega
kwa bega Serikali katika kuyafikia malengo yao hasa kwa sekta ya Afya.
Amesema (TAEC) itakuwa msimamizi na mshauri mzuri wa masuala
ya Atomu kwa wafanyakazi wa Zanzibar kuwajengea uwezo, kupata umahiri na
uweledi katika matumizi ya Nyuklia.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment