WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2024) amefanya ziara jijini Dodoma ili kukagua utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwenye taasisi zenye watu zaidi ya 100.
Waziri Mkuu ametembelea kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Makutupora (834 KJ), shule ya Sekondari Msalato na Gereza la Isanga ili kuona utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuwa taasisi zote za Serikali na binafsi zinazotumia nishati ya kuni kuandaa chakula cha watu zaidi ya 100 kwa siku zisitishe matumizi ya kuni na mkaa kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Desemba 31, 2024.
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dodoma na wa taasisi zote tatu kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo na yeye anapita kuangalia kama wamebadilisha mifumo inayotumika kwenye taasisi hizo.
“Nishati safi ya kupikia ni ubunifu wa Rais wetu ambaye amebobea katika masuala ya utunzaji mazingira, Rais wetu ametajwa kuwa ni kinara wa kampeni ya nishati safi barani Afrika. Tusije kushangaa akiwa kinara wa kampeni hii duniani, kwani ameshaenda Italia na Ufaransa kutoa mihadhara kuhusu nishati safi,” amesema.
“Kwa vile Afrika na dunia inamtambua, Watanzania tusibaki nyuma, na ndiyo maana tuliunda Kamati ya Kitaifa yenye wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Wakati kampeni hii inaendelea, tumetoa fursa kwa wajasiriamali kuanza biashara ya kuuza mitungi ya gesi, mkaa mbadala na KUNIPOA kama njia ya kuwatoa wananchi wetu kwenye nishati chafu ambayo ni kuni za kawaida na mkaa wa miti.”
Amesema majeshi, polisi, vyuo vya elimu ya kati na ya juu, vyuo vya wizara mbalimbali kama elimu, afya na kilimo ni baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kubadilisha mifumo yao ya kupikia kwani yana idadi kubwa ya watumiaji vya vyakula.
Alitumia fursa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini, wafanye ukaguzi kwa wajasiriamali wanaopika chakula cha watu wengi kama vile kwenye maharusi ili nao waweze kubadilisha mifumo yao ya kupikia. “Kupitia Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wa Dodoma ninawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini nendeni mkakague watu hao ili wabadilishe teknolojia zao, ziendane na matumizi ta nishati safi ya kupikia.”
Amesema ifikapo Desemba, mwaka huu wakuu hao watatakiwa watoe taarifa ya utekelezaji ikionesha ni taasisi ngapi tayari zimetekeleza agizo hilo. “Tunataka ifikapo Desemba, tujue taasisi ngapi tayari zimekamilisha, ngapi bado na mpango kazi ukoje wa taasisi hizo. Tunataka ifikapo mwaka 2033, tuwe na asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia.”
Mapema, akielezea utekelezaji wa programu hiyo kwenye makambi, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameanza kutumia mfumo wa nishati safi kwenye vikosi vyote 26 vya JKT.
Alisema JKT kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wanatekeleza mradi utakaowapatia majiko banifu na sufuria zake 291 kwa vikosi vyote, majiko ya gesi na sufuria zake 180, mitambo ya biogas tisa na majiko yake, mashine za kutengeneza mkaa mbadala 60 ambapo mafunzo kwa vijana kuhusu mitambo hii yataendeshwa na REA.
“Mradi wote utagharimu shilingi bilioni 5.7 ambapo REA watatoa shilingi bilioni 4.34 (asilimia 76) na JKT itachangia sh. bilioni 1.38 sawa na asilimia 24.”
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato, Mwl. Mwasiti Msokola alisema shule hiyo inatumia mkaa mbadala unaoitwa KUNIPOA ambao unatengezwa kwa kutumia maganda ya miwa, miti na pumba za mazao.
Alisema zamani walikuwa wakitumia sh. milioni 4.5 kila mwezi ili kununua kuni za kawaida, lakini kwa sasa wanaokoa sh. milioni 1.3 kwa kutumia KUNIPOA.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu alisema Jeshi hilo kwa kushirikiana na REA linatekeleza programu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani ambayo inahusisha vituo 211 ambapo kati ya hivyo magereza ni 129, ofisi 26 za Magereza za Mikoa na Vyuo vya Magereza vinne.
Alitaja vituo vingine kuwa ni Makao Makuu, Bohari Kuu, Hospitali kuu ya Jeshi, Karakana, Shule ya Sekondari Bwawani, Kikosi Maalum na Kambi za Magereza 47.
Alisema programu hiyo pia inahusisha utekelezaji wa miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa mitambo 126 ya Biogesi, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, ununuzi wa tani 865 za Mkaa Mbadala wa Rafiki; ununuzi wa mashine 61 za kutengeneza Mkaa Mbadala unaotokana na Mabaki ya Mazao na kuimarisha matumizi ya gesi asilia katika magereza ya Lilungu (Mtwara), Keko na Ukonga Complex (Dar es Salaam).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.
ALHAMISI, NOVEMBA 7, 2024.
No comments:
Post a Comment