Habari za Punde

MAAFISA HABARI MSIWE CHANZO CHA KUPOTOSHA MUUNGANO: MITAWI

 

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi amewanasihi Maafisa habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kuhakikisha nyaraka wanazoziandika za taasisi zao haziwi chanzo cha kupotosha Muungano badala yake watumie vyema taaluma zao kwa kuhubiri mazuri yanayohusu Muungano wa Tanzania.

Bw. Mitawi ametoa nasaha hizo alipozungumza na Maafisa hao, ukumbi wa Zanzibar School of Health (ZSH), Mombasa kwa Mchina, Wilaya ya Magharibi  B, Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye mafunzo ya kimkakati yaliyojadili masuala ya Muungano.

Akizungumzia suala la ufanisi kwa Taasisi wanazozitumikia maafisa hao, Mitawi aliwaeleza kukosekana kwa ufanisi kwenye taasisi zao ni udhaifu wa vitengo vyao vya habari, hivyo aliwashauri kuwa weledi na kuitumikia vyema tasnia yao hasa katika kuzieleza faida za Muungano.

Katika hatua nyengine, Mitawi waliwasifu Maafisa hao kwamba wao ni daraja muhimu la kulinda na kukuza hadhi na heshima za taasisi zao, hivyo aliwataka kuwa kama macho ya kuangaza mazuri na mabaya yanayoelekezwa kwenye taasisi zao pamoja nakuwasihi kuwa pua itakayonusa taarifa zinazohusu taasisi zao kwa kufanyia kazi watakayoyapata pia kuwa kama masikio ya kusikiliza kila kinachoelekezwa kwenye taasisi wanazozitumikia.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZICOO), Bi. Raya Hamad Mchwere ameeleza mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea maarifa maafisa hao ambao ni daraja kati ya Serikali za SMZ na SMT na taasisi zao ambao wanasaidia kuwafikishia wananchi yale yote yanayofanywa na Serikali hizo.

Naye, Katibu wa ZICOO Bw. Makame Khamis Moh’d lengo la Jumuiya hiyo mbali ya kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili lakini kuwakumbusha wajibu wao kwa taasisi wanazozitumikia.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyojadili masuala ya Muungano yaliandaliwa na Jumuiya ya Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano ya Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar (ZICOO) kwa udhamini wa Ofisi ya Makamu wa Rais na taasisi ya Zanzibar School of Health (ZSH) ambapo mada mbili zilizojadili masuala ya Muungano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanznibar, (SUZA) zilijadiliwa. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ofisi ya ya Zanzibar, imeshiriki kwenye mafunzo hayo.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.