Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Azungumza na Wananchi wa Muhugoni - KIWANI

Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema yeye na wenzake wanayo adhma ya dhati ya kuwatumikia wananchi wote wa jimbo hilo kwa  usawa pasipo kujali itikadi zao za kisiasa.

Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na kuomba kura kwa wannachi wa kijiji cha Mchakwe pamoja na Wakulima, wafugaji na wavuvi waliomo katika kijiji cha kiwani Maambani Pemba.

Amesema watakapo pata ridhaa ya kuchaguliwa kuwa viongozi wa jimbo hilo watahakikisha wanayaendeleza  yale yote mazuri yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, hospitali na uwezeshwaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kujikwamua na umasikini.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa wanawake wa jimbo la kiwani watapatiwa elimu ya ujasiri amali, mitaji na mikopo isiyo na riba sambamba na kusimamia upatikanaji wa masoko ya kuuzia biashara zao ndani na nje ya nchi.

Amewatoa hofu vijana katika jimbo la kiwani kwa kuwaahidi kuwa mara baada ya kuwa mwakilishi wa jimbo hilo atasimamia upatikanaji wa ajira kwa vijana kwa kutafuta mbinu mbadala za kuweza kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe ili kujikwamua na maisha.

Amesema makundi yote yataangaliwa ikiwemo wavuvi, wakulima, wafugaji na  wajasiriamali kwa kupatiwa elimu, mitaji na nyenzo za kufanyia shughuli zao ili kuweza kupata mazao yenye tija na faida kubwa.

Sambamba na hayo Ndugu  Hemed amesema wamejipanga kuboresha na kuimarisha miundombinu katika sekta ya elimu na afya ili kuhakikisha huduma zote muhimu, matibabu na madawa  yanapatikana bila ya malipo yoyote jimboni humo.

Amewataka wazee wenye watoto walio na mahitaji maalum (walemavu) kuacha tabia ya kuwafungia ndani na kuwakosesha kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu, afya na nyenginezo hivyo atakapokuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiwani atahakikisha watoto hao  wanapatiwa huduma zote stahiki na muhimu kwa maisha yao.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kiwani ndugu Hija Hassan Hija amesema lengo la kugombea kwake ni kutaka kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kiwani kwa  utumishi uliotukuka kwa nia thabiti ya kuwaletea maendeleo jimboni humo.

Ndugu Hija amesema Akipata ridhaa ya kuwa Mbunge wa jimbo la kiwani atajenga diko na soko la kisasa jimboni humo ili kurahisisha harakati za uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla jambo litakalotanua harakati za kiuchumi jimboni humo.

Amesisistiza kuwa uchangiaji wa  ada kwa wananfunzi wa Jimbo la kiwani utabaki kuwa historia na wanafunzi wote watagharamiwa na viongozi wao wa Jimbo ili kutoa nafasi kwa wananfunzi kujisomea  pasipo na usumbufu wowote.

Kwa upande wake mgombe wa udiwani wadi ya Kendwa ndugu Ali Abdalla Ali amewataka vijana wa Jimbo la Kiwani kuendelea kuitunza amani na mshikamano uliopo nchini na kukataa kutumika kuwa chanzo chanuvunjifu wa amani.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.