Serikali imesema inajiandaa kumaliza tatito la upatikanaji vyeti vya kuzaliwa watoto, lililodumu kwa muda mrefu sasa.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, aliyasema hayo barazani jana wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Kojani, Hassan Hamad Omar, aliyetaka kujua ni kwanini tatizo la uchelewaji vyeti vya kuzaliwa bado linaendelea na kwanini serikali inashindwa kutoa vyeti hivyo katika kipindi kifupi.
Alisema serikali imeanza kukabiliana na tatizo hilo kwa kutumia utaratibu wa kutoa vyeti hivyo ndani ya kipindi cha wiki mbili baada ya watoto kuzaliwa.
Alisema hivi sasa maeneo ambayo tayari wameanza kuyafanyiakazi ni pamoja na Wilaya ya Magharibi Unguja, Wilaya ya Mjini, Micheweni, Kaskazini ‘B’ na Kusini Unguja.
Alieleza kwamba Wizara hiyo pia inaimarisha mifumo ya usajili wa Vizazi na vifo ikiwa ni hatua itakayoweza kupunguza tatizzo la uchelewaji wa utoaji vyeti.
Alisema jambo jengine linalotayarishwa na serikali ili kuboresha huduma hiyo ni pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria ya vizazi na vifo, sheria ya ndoa na talaka kwa kuifanya kuwa ni moja.
Alisema katika kuitekeleza kazi hiyo, wizara hiyo imeanza kujifunza mfumo mpya wa kutoa vyeti hivyo na utunzaji kwa kufuata utaratibu uliotumika katika nchi za Sychelles na Norway.
1 Comments
Wizara isiishie hapo, iangalie pia suala la kufanana kwa vyeti vyenyewe(uniformity).kuna watu vyeti vyao vina mihuri ya jamhuri ya muungano(Adam na Hawa) pale juu. Kuna wengine vina mihuri ya SMZ.( visiwa,Mnazi, mkarafuu,panga na shoka) Mihuri ya chini mingine ya moto ,mingine ya wino. Kuhusu majina kunatakiwa pia kuwe na 'uniformity' Maafisa wawe na elimu ya kujua asili za majina.vipi utakubali kumuandika mtoto jina SALUMU wakati asili ya jina ni SALIM kwa vile tuu, mzazi wake ndivyo alivyo litamka au kuliandika kwa mara ya kwanza..wazee wengine huwa hawajui hayo..wasaidieni!
ReplyDelete