Matumaini ya Morocco Chalenji yako juu
Na Mwandishi Wetu
FUNGU la kwanza la timu ya taifa ya soka 'The Zanzibar Heroes', limeondoka jana asubuhi kwenda nchini Misri kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na mashindano ya Chalenji mwaka 2011.
Msafara wa timu hiyo ulioongozwa na Ofisa Michezo Mkoa wa Kaskazini Unguja Faida Salmin Juma, uliondoka kwa ndege ya shirika la Kenya Airways bila ya wachezaji wake mahiri ambao pia wanachezea timu ya taifa Tanzania 'Taifa Stars'.
Wachezaji hao walioachwa, ambao wanasubiri mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Chad wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil, ni mlinda mlango Mwadini Ali, Nassor Masoud 'Cholo', Aggrey Morris na Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye hata hivyo ameenguliwa katika kikosi cha Stars akikabiliwa na majeraha.
Imefahamika kuwa, wachezaji hao watakwenda Cairo Novemba 16 kuungana na wenzao, mara baada ya pambano hilo la Stars litakalochezwa jijini Djamena Novemba 16, huku kocha mkuu wa Zanzibar Heroes Stewart John Hall, akitarajiwa kukifuata kikosi chake kesho.
Mbali na nyota hao, Heroes haina uhakika wa kumpata nahodha wake Abdi Kassim 'Babi', ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Vietnam, kwa kile kilichoelezwa kuwa klabu anayochezea haijampa kibali cha kuondoka hadi habari hizi zinaandikwa.
Wakati timu hiyo ikiondoka jana, msaidizi kocha mkuu Hemed Suleiman 'Moroko', alieleza matumaini yake kuwa kambi ya Cairo na mechi za kupima nguvu watakazocheza, zitasaidia kuwafanya wachezaji wazoeane, hasa kutokana na muda mchache walioupata kuwa pamoja.
"Nadhani wiki mbili za kuweko Cairo, zinatosha kuwaimarisha wachezaji wetu, na bila shaka wakati wa mashindano ya Chalenji watakuwa fiti kufanya kile walichotumwa na taifa lao", alijipa moyo kocha huyo.
Ikiwa nchini Misri, timu hiyo itacheza mechi sita na klabu zinazocheza ligi kuu nchini humo pamoja na timu ya taifa ya vijana walio chini ya miaka 23.
Kabla ya kuondoka jana na kuagwa na maofisa mbalimbali wa mamlaka za michezo nchini, timu hiyo ilicheza mechi ya kirafiki katika uwanja wa Mao Dzedong, na kutoka sare ya kutokufungana.
0 Comments