WAISLAMU wametakiwa kushikamana katika dini ya Mwenyezi Mungu (uislamu ) na wasifarakane, kwani kwao kunaleta faida kubwa ya kumuabudu Allah kwa wingi jambo ambalo litaleta faida ndani yake.
Umoja katika Shughuli yoyote ni Silaha kubwa na ya pekee katika kukuza amani ndani ya dunia na mifarakano itawapa fursa maadui zao kuwahujumu iwe katika dini ama shughuli nyengine za kijamii.
Kutafautiana kwa misngi ya ukubwa wa madaraka, mali, rangi ,wala ukabila ni vitu visivyomsaidia Mja katika maisha yake yawe ya duniani wala akhera isipokuwa kitakachomfaa ni kufanya amali kwa wingi na hiyo itapatikana kwa kuwa kitu kimoja kama waislamu ambao kwa sasa wako Makka wakifanya amali mbali mbali kwa ajili ya kutafuta shufaa kwa Allah.
Hayo yalielezwa na Sheikh, Ali Said Ali wa Masjid Huda ya Machomanne Pemba, aaiposoma Khutba ya Sala ya Iddi Kitaifa iliyofanyika kiwanja cha nje ya Gombani mpya, Sala ambayo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein na waumini mbali mbali wa dini ya kiislamu kisiwani humo.
Alisema ni vyema waislamu wakaithamini neema kubwa waliyopewa na Mwenyezi Mungu ya uislamu, dini ambayo imetandika kila mambo mema ambayo ataeyafanya hupata malipo mema na ya kudumu mbele ya Mola wake.
“Waislamu tukumbuke Mwenyezi Mungu (SWT) ametuumba kwa ajili moja tu ya kumuabudu, hivyo hatunabudi kutekeleza kwa dhati yale aliyotuamrisha ili tupate malipo mema na ya milele” aliusia Sheikh Ali.
Aliendelea kusema kuwa mwenye kumtii Allah kikweli kweli na kufanya mambo mema basi huwa ameongoka katika kheri kubwa hivyo ni lazima waislamu wamuogope Mweyezi Mungu kwa kuacha kufanya mambo ambayo Mwenyezi Mungu anayapenda.
Sheikh Ali Said, alieleza kuwa waislamu wakati huu wako katika Ibada ya Hijja huko Makka na wanafanya amali kubwa na wale ambao hawakubahatika basi wamuombe Allah msamaha ili wapate kheri kubwa.
“Mwenye kufanya amali ya Hijja na isiingize jambo lolote baya ndani yake ni mfamo wa mtu aliekuwa anazaliwa sasa hana dhambi” alinukuu.
Aidha aliwataka Waislamu wenye Uwezo wa kuchinja kuitumia siku hii kwa kufanya tendo hilo la kuchinja na kutowa Sadaka kwa wale wasio na Uwezo, ili kuinasibisha siku hiyo na mtihani mkubwa ambao Allah alimpa Mtume wake Nabii Ibrahim wakati alipooteshwa katika ndoto kumdhahi mtoto wake.
Alisema waislamu ni vyema siku hii wakaisherehekea kwa kufanya mambo mema na kuacha kabisa kufanya mambo ambayo yatamkasirisha Mwenyezi Mungu na wajiepushe sana na kumshirikisha na kitu chengine.
Aliwataka waislamu kujiepusha na ghadhabu za Allah kwa kusema uongo, kula rushwa, Hasadi, kusengenya, kuiba, kuzini n.k, kwani ni vitendo ambavyo anavichukia, na atamuadhibu mja wake kwa kutenda hayo.
Hivyo aliwasisitiza waislamu kuwa kitu kimoja na kushirikiana na kuacha tafauti zao mbali mbali kwani umoja wao utawaletea faida kubwa ya kimaendeleo na watakuwa na nguvu ya pamoja ya kumuabudu Mwenyezi Mungu.
0 Comments