6/recent/ticker-posts

NAHODHA AWASHANGAA WAPENDA MAANDAMANO

Na Kunze Mswanyama, Dar

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, amesema hafurahishwi na matumizi ya vifaa vinavyotumika katika kutuliza ghasia hasa ikizingatiwa kuwa wahusika ni watu wenye akili timamu.

Nahodha alisema hayo jijini Dar es Salam, alipokuwa akijibu masuali kutoka kwa waandishi wa habari na kuulizwa anaisikiaje jeshi la polisi kutumia risasi za moto katika kuzuia ghasia badala ya zile za mpira ambazo mara nyingi huwa hazisababishi vifo.


Alisema ni jambo la kusikitisha na kusononesha juu ya tabia inayojengeka ya kufanya mambo bila ya kufuata sheria jambo linalosababisha serikali kupitia jeshi la polisi kuzuia uhalifu huo.

Alisema kwa vile wahusika wote ni binadamu ambao wamependelewa akili ambazo wanyama hawakupewa, hivyo kutotii sheria huonekana kama wanajitakia kupigwa mabomu, kurushiwa maji ya kuwasha jambo ambalo alibainisha kuwa ni la kusikitisha.

Nahodha aliwataka wananchi kutotumia mwanya kudai demokrasia kwa kufanya mandamano yasiyokuwa na kibali kwani yanaweza kutumiwa na wahalifu kutekeleza azma zao.

Waziri huyo aliendelea kufahamisha kuwa kasi yake ya kutowavumulia wafanyakazi wazembe ataendelea kuwa nayo ambapo ameshazungumza na wakuu wa Idara zote.

Akizungumzia maslahi kwa watumishi wa wizara hiyo, alisema tayari wamekwisha pendekeza serikalini kuongeza posho za askari wa polisi, magereza na zima moto ili kuwaongezea ari ya utendaji kazi wao.

“Tumependekeza ongezeko la posho ya shilingi 150,000 kutoka 100,000 iliyoanza kutumia miaka mingi iliyopita hivyo kama serikali itakuwa na uwezo itatupa katika bajeti hii kama haina basi tutasubiri bajeti ijayo”, alisema.

Post a Comment

0 Comments