Na Aboud Mahmoud
WANANCHI wanaoishi katika Wilaya ya Magharibi Unguja,wametakiwa kuwa makini katika kudhibiti maeneo ili kuweza kusaidia katika kuweka ardhi ya kilimo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi,Hassan Mussa Takrima,wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wananchi wa shehia mbali mbali za wilaya hiyo yalioandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhi Mazingira Zanzibar(CODECOZ) katika ukumbi wa Elimu Mbadala.
Alisema maeneo mengi ya ardhi katika visiwa vya Unguja yameweza kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuondosha maeneo ya kilimo hali inayohatarisha kutoweka kwa kilimo nchini.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa ingawa ardhi ni ndogo na wananchi wamekuwa wengi,bado wananchi hao hawana budi kujenga nyumba za ghorofa ili kuinusuru ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo.
Nae Katibu wa CODECOZ,Kapten Hamza Makame Omar,alisema jumuiya hiyo imejipanga kuweka mazingira safi katika maeneo ya Unguja na Pemba kwa kushirikiana na wananchi.
Alieleza kuwa CODECOZ, imefanikiwa kutoa mafunzo kwa watu mbali mbali wakiwemo masheha,madiwani,wajumbe wa kamati za shehia pamoja na wananchi.
0 Comments