6/recent/ticker-posts

WATATU YOUNG ELEVEN KIFUNGONI MWAKA MMOJA

Na Abdi Suleiman, Pemba

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mkoani, kimewafungia wachezaji watatu wa timu ya Young Eleven wasishiriki mashindano yoyote kwa msimu mzima wa mwaka 2011/12, baada ya kuwatia hatiani kwa kitendo cha kumpiga muamuzi Faki Khatib Kombo.

Wachezaji waliokumbwa na kifungo hicho, ni Hemed Abdalla, Nasir Hamad na Abeid Mohammed, pamoja na mlezi wa timu hiyo aliyetajwa kwa jina la Wahid, ambaye amepewa adhabu ya kutohudhuria mchezo wowote utakaohusisha timu yake ambao utaandaliwa na chama hicho.


Uamuzi huo umo ndani ya barua ya ZFA wilayani humo, iliyotumwa kwa uongozi wa klabu ya Young Eleven, hatua iliyochukuliwa na kamati tendaji ya ZFA Novemba 3, mwaka huu.

Wanandinga hao wamedaiwa kufanya vitendo vya kihuni wakati timu yao ilipocheza dhidi ya Black Wizard ukiwa mchezo wake wa kwanza wa ligi daraja la pili wilaya, uliofanyika kwenye uwanja wa Mkanyageni.
Imeelezwa kuwa mchezo huo ulianza kuharibika katika dakika ya 63, baada ya timu ya Young Eleven kuanza kufanya vitendo vya kihuni vilivyodaiwa kuhatarisha amani uwanjani hapo.

Aidha ZFA Wilaya ya Mkoani, imeelezea kusikitishwa kwake na uongozi wa timu hiyo kushindwa kuwazuia wachezaji na mashabiki wake wasifanye vurugu, na kusababisha muamuzi Faki Khatib Kombo kupigwa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu, huku akipoteza baadhi ya vitu vyenye thamani ya shilingi 30,500.

Katika barua hiyo, kamati tendaji ya ZFA imesema kuwa, imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote ikiwemo ripoti ya muamuzi wa mchezo, msimamizi na kamisaa.

Pamoja na kuwasweka jela wachezaji hao, ZFA pia imeipiga klabu hiyo faini ya shilingi 30,500, ikiwa thamani ya vifaa vya muamuzi vilivyopotea, sambamba na faini ya shilingi laki tatu, ikitakiwa kulipa nusu yake kabla ya Disemba 3 mwaka huu, na kiasi kitakachobaki kabla ya Januari 7, mwakani.

ZFA imesema, endapo timu hiyo itashindwa kulipa faini hiyo hadi tarehe ya mwisho, haitasita kuitoa katika mashindano ya mwaka huu pamoja na kuiteremsha katika daraja la tatu msimu ujao.

Post a Comment

0 Comments