Na
Salum Vuai, Maelezo
KAMA
mikakati madhubuti haitachukuliwa kudhibiti matumizi mabaya ya ardhi, Zanzibar inaweza kupoteza
kabisa maeneo ya kilimo katika miaka 50 ijayo.
Tahadhari
hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Dk. Juma
Ali Juma, alipofungua warsha ya kujadili rasimu ya sera mpya ya ardhi
iliyofanyika katika ukumbi wa ASSP Maruhubi mjini Zanzibar.
Dk.
Juma alisema, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu hapa nchini, kumekuwa
na mahitaji makubwa ya ardhi yanayosababisha watu hao kuvamia maeneo muhimu
yakiwemo ya kilimo na vianzio vya maji.
Katika
warsha hiyo iliyoshirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya ardhi kutoka taasisi
na jumuiya tafauti, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema wakati sera ya sasa ya ardhi
ikianzisha miaka 20 iliyopita, idadi ya wakaazi wa Zanzibar ilikuwa 649,000,
lakini kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi hiyo imepaa na kufikia watu
1,303,568.
Alieleza
kuwa, kumekuwa na matumizi mabaya ya ardhi kwa vile watu wanavamia maeneo
muhimu yakiwemo ya hifadhi ya misitu na kufanya shughuli za kujiendeleza kimaisha,
lakini bila kuzingatia umuhimu wa kuitunza hali inayohatarish
a kupotea kwa
ardhi ya kilimo katika kipindi kifupi kijacho.
“Mahitaji
ya ardhi kwa shughuli za kilimo, majenzi na miundombinu mbalimbali yamezidi
kutokana na ongezeko la watu, hili haliwezi kuepukika lakini ni vyema matumizi
hayo yazingatie mahitaji mengine ya lazima”, alifafanua.
Aidha,
alifahamisha kuwa, ardhi haiwezi kutanuka na kukidhi mahitaji, bali kinyume
chake hapa Zanzibar, ardhi imekuwa ikipungua kutokana na mabadiliko ya tabia
nchi, ambapo maeneo ya kilimo katika baadhi ya vijiji, hayawezi kutumika tena
kutokana na kuvamiwa na maji ya bahari.
Alitanabahisha
kwa kusema, ni lazima kuwe na mikakati madhubuti, ili sera mpya ya ardhi
yatambue maeneo ya rasilimali muhimu kama na kuweka mipaka ya ardhi ya kilimo,
mifugo, vianzio vya maji na maeneo ya ujenzi wa makaazi.
Akifafanua
zaidi, Dk. Juma alisema kutokuwepo mipaka kama hiyo, ndio maana mito mingi
iliyokuwa ikipita chini ya madaraja mbalimbali hapa nchini, imekauka kwa kuwa
watu wameamua kuivamia na kujenga nyumba za kuishi pamoja na kufanya biashara.
Alitoa
mfano wa daraja lililoko Kinazini mjini Unguja, Saateni, Mtoni na Bububu, kuwa
ni ushahidi wa athari zitokanazo na utashi wa binadamu na kutokuwepo mipango
mizuri ya kudhibiti matumizi mabaya ya ardhi nchini.
“Kutokana
na kupungua ardhi ya kilimo kwa uvamizi, inasikitisha kuona nchi inaagiza
makontena mengi ya ‘mapembe’ (mchele), lakini kama
hatutakuwa makini, ninapata hofu kuwa baada ya miaka 50 ijayo, tutakuwa tunaagiza
makontena ya maji kutoka nje”, alitoa tahadhari.
Alisema
ni lazima wananchi wajifunze namna ya kuitumia vyema ardhi ndogo iliyopo
Zanzibar kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, ili kuinusuru nchi na janga
la kimazingira.
Akitoa
mada katika warsha hiyo, ofisa kutoka Idara ya Kilimo Ramadhani Othman, alisema
kila mmoja anategemea ardhi kwa maendeleo, hivyo hakuna budi kuitunza,
kuihifadhi na kuitumia kwa malengo maalumu.
Alisema
asilimia 80 ya wakaazi wa Zanzibar wanategemea kilimo moja kwa moja au
vyenginevyo, lakini wakulima wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kupungua kwa
ardhi ya kilimo.
Naye Mshauri Elekezi ambaye ni Mwanasheria, Omar
Sururu Khalfan, alisema sera ya ardhi inapaswa kuzingatia haja ya kupunguza
migogoro ya ardhi ambayo kila siku inaongezeka na kutishia amani kati ya
wanajamii.
Warsha hiyo imeandaliwa na Jumuiya ya UHAI
inayojishughulisha kutoa elimu kwa wadau wa ardhi, wakiwemo wakulima na
wafugaji, na kuandaliwa na taasisi ya BEST-AC kutoka Dar es Salaam.
1 Comments
Ama kweli "Msema pweke hakosei" hivi kweli jamani tuseme SMZ hawajui kua Z'bar hakuna mtu anae vamia ardhi au watendaji wetu ni wavivu wa kutafuta mbadala wa neno 'kuvamia'?
ReplyDeleteTatizo kubwa la Z'bar ni kwamba Wananchi wanauza mashamba yao na heka walizopewa na SMZ wanavyotaka wenyewe kwa vile hakuna sheria wala mwongozo unaotolewa na serikali juu ya wapi wauze na wapi wasiuze!
Tena viongozi wa SMZ walivyo wa ajabu hata na wao wenyewe utakuta wananunua humo humo!
Hao masheha ndio kabisa wanashindwa hata kuwashauri wauzaji wa viwanja waache njia..wapo wapo tu!
Ndio maana wakati baadhi ya Wazanzibari wakidai mamlaka zaidi VISIWANI mimi mwenzenu, huona bora wapunguziwe, wasije wakatilisha 'MAVI'