6/recent/ticker-posts

Ardhi ya kilimo hatarini kutoweka



Na Salum Vuai, Maelezo
KAMA mikakati madhubuti haitachukuliwa kudhibiti matumizi mabaya ya ardhi, Zanzibar inaweza kupoteza kabisa maeneo ya kilimo katika miaka 50 ijayo.

Tahadhari hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Dk. Juma Ali Juma, alipofungua warsha ya kujadili rasimu ya sera mpya ya ardhi iliyofanyika katika ukumbi wa ASSP Maruhubi mjini Zanzibar.

Dk. Juma alisema, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu hapa nchini, kumekuwa na mahitaji makubwa ya ardhi yanayosababisha watu hao kuvamia maeneo muhimu yakiwemo ya kilimo na vianzio vya maji.

Katika warsha hiyo iliyoshirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya ardhi kutoka taasisi na jumuiya tafauti, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema wakati sera ya sasa ya ardhi ikianzisha miaka 20 iliyopita, idadi ya wakaazi wa Zanzibar ilikuwa 649,000, lakini kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi hiyo imepaa na kufikia watu 1,303,568.

Alieleza kuwa, kumekuwa na matumizi mabaya ya ardhi kwa vile watu wanavamia maeneo muhimu yakiwemo ya hifadhi ya misitu na kufanya shughuli za kujiendeleza kimaisha, lakini bila kuzingatia umuhimu wa kuitunza hali inayohatarish
a kupotea kwa ardhi ya kilimo katika kipindi kifupi kijacho.

“Mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kilimo, majenzi na miundombinu mbalimbali yamezidi kutokana na ongezeko la watu, hili haliwezi kuepukika lakini ni vyema matumizi hayo yazingatie mahitaji mengine ya lazima”, alifafanua. 

Aidha, alifahamisha kuwa, ardhi haiwezi kutanuka na kukidhi mahitaji, bali kinyume chake hapa Zanzibar, ardhi imekuwa ikipungua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo maeneo ya kilimo katika baadhi ya vijiji, hayawezi kutumika tena kutokana na kuvamiwa na maji ya bahari.

Alitanabahisha kwa kusema, ni lazima kuwe na mikakati madhubuti, ili sera mpya ya ardhi yatambue maeneo ya rasilimali muhimu kama na kuweka mipaka ya ardhi ya kilimo, mifugo, vianzio vya maji na maeneo ya ujenzi wa makaazi.

Akifafanua zaidi, Dk. Juma alisema kutokuwepo mipaka kama hiyo, ndio maana mito mingi iliyokuwa ikipita chini ya madaraja mbalimbali hapa nchini, imekauka kwa kuwa watu wameamua kuivamia na kujenga nyumba za kuishi pamoja na kufanya biashara.

Alitoa mfano wa daraja lililoko Kinazini mjini Unguja, Saateni, Mtoni na Bububu, kuwa ni ushahidi wa athari zitokanazo na utashi wa binadamu na kutokuwepo mipango mizuri ya kudhibiti matumizi mabaya ya ardhi nchini.

“Kutokana na kupungua ardhi ya kilimo kwa uvamizi, inasikitisha kuona nchi inaagiza makontena mengi ya ‘mapembe’ (mchele), lakini kama hatutakuwa makini, ninapata hofu kuwa baada ya miaka 50 ijayo, tutakuwa tunaagiza makontena ya maji kutoka nje”, alitoa tahadhari. 

Alisema ni lazima wananchi wajifunze namna ya kuitumia vyema ardhi ndogo iliyopo Zanzibar kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, ili kuinusuru nchi na janga la kimazingira.

Akitoa mada katika warsha hiyo, ofisa kutoka Idara ya Kilimo Ramadhani Othman, alisema kila mmoja anategemea ardhi kwa maendeleo, hivyo hakuna budi kuitunza, kuihifadhi na kuitumia kwa malengo maalumu.

Alisema asilimia 80 ya wakaazi wa Zanzibar wanategemea kilimo moja kwa moja au vyenginevyo, lakini wakulima wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kupungua kwa ardhi ya kilimo.

Naye Mshauri Elekezi ambaye ni Mwanasheria, Omar Sururu Khalfan, alisema sera ya ardhi inapaswa kuzingatia haja ya kupunguza migogoro ya ardhi ambayo kila siku inaongezeka na kutishia amani kati ya wanajamii.

Warsha hiyo imeandaliwa na Jumuiya ya UHAI inayojishughulisha kutoa elimu kwa wadau wa ardhi, wakiwemo wakulima na wafugaji, na kuandaliwa na taasisi ya BEST-AC kutoka Dar es Salaam. 

Post a Comment

1 Comments

  1. Ama kweli "Msema pweke hakosei" hivi kweli jamani tuseme SMZ hawajui kua Z'bar hakuna mtu anae vamia ardhi au watendaji wetu ni wavivu wa kutafuta mbadala wa neno 'kuvamia'?

    Tatizo kubwa la Z'bar ni kwamba Wananchi wanauza mashamba yao na heka walizopewa na SMZ wanavyotaka wenyewe kwa vile hakuna sheria wala mwongozo unaotolewa na serikali juu ya wapi wauze na wapi wasiuze!

    Tena viongozi wa SMZ walivyo wa ajabu hata na wao wenyewe utakuta wananunua humo humo!

    Hao masheha ndio kabisa wanashindwa hata kuwashauri wauzaji wa viwanja waache njia..wapo wapo tu!

    Ndio maana wakati baadhi ya Wazanzibari wakidai mamlaka zaidi VISIWANI mimi mwenzenu, huona bora wapunguziwe, wasije wakatilisha 'MAVI'

    ReplyDelete