Na Husna Mohammed, Beijing
SERIKALI ya Jamhuri ya watu wa China imetumia dola trilioni moja kwa ajili ya kujenga miundombinu ya mtandao wa mawasiliano ya barua pepe (Internet) nchini humo.Akiwasilisha mada juu ya utawala na maendeleo ya intenet ya China katika mafunzo ya wanahabari yanayoendelea mjini hapa, Mtafiti kutoka chuo cha Sayansi ya Jamii China, Min Da Hong, alisema kuwa fedha zimetumika kwa ajili ya kujenga mawasiliano mbalimbali ikiwa ni pamoja na barua pepe, twitter, mawasiliano ya moja kwa moja (on line),facebook (Weibo) na kadhalika.
Min Da Hong, alisema pamoja na mambo mengine China imepiga hatua ya kimaendeleo kutokana na matumizi ya mawasiliano ya Intanet.
Aliyataja maeneo yanayoongoza kwa matumizi ya intanet nchini humo kuwa ni pamoja na Beijing, Shanghai, Guangdong ambapo asilimia 70 ya intanet yamekuwa yakitumika kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi.
Aidha aliongeza kuwa matumizi ya intanet yamekuwa yakitofautiana kutoka mkoa na mkoa, mjini na vijijini.
Alifahamisha kuwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani shughuli nyingi za kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kiutamaduni matumizi zimekuwa zikikua kutokana na mawasiliano ya aina hiyo kukua siku hadi siku.
“Hadi sasa China ina mtaji wa zaidi ya dola bilioni 2 kwa makampuni mbalimbali ya mawasiliano”, alisema.
Sambamba na hilo, Min Dahong alisema matumizi makubwa ya intanet yamekuwa yakitumika katika vyombo vya habari ikiwemo, magazeti, radio, televisheni matumizi mengine ya mawasiliano na hata filamu.
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa matumizi ya intanet, Min Dahong, alisema hali hiyo imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba matumizi ya lugha chafu, matusi, ugaidi, uhalifu ni mambo yaliyodhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
“Taasisi inayoshughulikia mawasiliano ya intanet imekuwa ikihakikisha hakuna lugha chafu wala vitisho kwa kuwa miundombinu ya mawasiliano yamedhibitiwa ipasavyo”, alisema.
Hadi kufikia Disemba mwaka 2012, zaidi ya watu milioni 100 nchini China wamekuwa wakitumia mtandao kwa kupitia simu za mkononi ambapo kati yao milioni 82.6 wanatumia simu za aina ya 3G.
Aidha, alisema ili kuona nchi hiyo inaendelea zaidi matumizi ya mtandao yataweza kuimarishwa sehemu za vijijini nchini humo.
0 Comments