Na Mwandishi wetu, Moshi
KESI ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya (43), imelazimika kusikilizwa chumbani baada ya kutokea sintofahamu huku mmoja wa waandishi wa habari aliyekuwa akifuatilia kesi hiyo akishambuliwa na ndugu wa marehemu.
Kesi hiyo iliyotajwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi, Agosti 21 mwaka huu, ilipangwa tena kusikilizwa katika mahakama ya wazi jana lakini kutokana na kuwepo kwa umati mkubwa mahakamani, kesi hiyo ilihamishiwa mahakama ya ndani jambo lililowakera ndugu wa marehemu ambao walianza kufanya vurugu na kulazimisha askari wa mahakama kuingilia kati wakisaidiwa na wale wa kutuliza ghasia (FFU).
Katika tukio hilo, waandishi wa habari wachache walioruhusiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo walijikuta katika wakati mgumu, huku mmoja wao, Venance Maleli wa kituo cha redio cha Moshi FM akishambuliwa na wanandugu hao ambao pia walitishia kumnyang’anya kamera yake.
Tukio hilo halikuishia hapo kwani hata mwandishi mwengine alifanyiwa fujo na ndugu wa marehemu ambao hawakutaka kupigwa picha wakati wakifanya juhudi za kumkimbiza hospitalini mama yao, aliyepoteza fahamu baada ya kupata taarifa za kuahirishwa kesi hiyo.
Aidha baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa mahakamani hapo walilazimika kuondoka kwa kujificha kwa kuhofia usalama wao.
Wananchi waliokuwepo nje ya mahakama walishangazwa na wanafamilia wa marehemu kuwanyanyasa wanahabari ambao wanawasaidia wao kutangaza maendeleo ya kesi hiyo ili haki itendeke.
"Hivi wanahabari wakiamua kususia kuripoti kesi hii wanadhani itakuwaje? hivi hawajui kuwa kesi hii inapewa uzito kwa kuwa wanahabari wanaifuatilia kwa karibu?" walisikika baadhi ya wananchi waliofurika katika mahakama hiyo wakisema.
Katika kesi hiyo washtakiwa wengine wanne waliunganishwa katika shtaka hilo la mauaji kwa kukusudia kinyume na kanuni namba 16, kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya jinai.
Washtakiwa hao ni Joseph Damas maarufu Chusa mkazi wa Jijini Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati,Sadiki Mohammed Jabir (32) mkazi wa Dar es Salaam na Langata wilayani Hai na Karim kihundwa (33) mkazi wa kijiji cha Lawate wilayani Siha na kufanya jumla ya washtakiwa kufikia saba.
Hata hivyo, maelfu ya wananchi waliofurika mahakamani hapo hawakupata fursa ya kuwaona washtakiwa baada ya mahakama kuamua kuisikiliza chumbani.
Baada ya kusomewa tena mashtaka yao washtakiwa waliondolewa mahakamani hapo kwa ulinzi mkali wa polisi waliotumia gari la vioo vya kiza lenye namba za usajili T 743 ADC.
Katika kesi hiyo Jamhuri inasimamiwa na wakili wa serikali Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sikule chini ya hakimu mkazi, Ruth Mkisi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 2 kwa ajili ya kutajwa tena.
0 Comments