Na Salum Vuai, Maelezo
WATU watatu kati ya watano waliokamatwa na jeshi la Polisi Zanzibar wakishukiwa kuwa ni wahamiaji haramu, wamethibitika kuwa ni raia halali wa Tanzania.Hata hivyo, watu hao watano ndio pekee waliokabidhiwa Idara ya Uhamiaji kutoka Makao Makuu ya Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, licha ya jeshi hilo kutangaza kukamata watu kumi mwanzoni mwa wiki.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwanakwerekwe, Mwanasheria wa Idara ya Uhamiaji, Tahir Khamis Mussa, alisema watu wote waliofikishwa idarani hapo, wakati wa kuhojiwa walidai kuwa wao si wahamiaji haramu bali ni raia wa Tanzania.
Alisema, hadi akitoa taarifa hii, idara yake ilikuwa imeridhika na vielelezo vilivyooneshwa na watatu kati yao, huku wengine wawili wakipewa muda hadi jana Alkhamisi, kupeleka vielelezo kamili vitakavyothibitisha uraia wao.
Mwanasheria huyo aliwataja watu hao watatu kuwa ni Stephen Vitus Manda, ambaye alionesha pasi ya kusafiria ya Tanzania, iliyotolewa Dar es Salaam Machi 20 mwaka huu, pamoja na cheti cha kuzaliwa kinachoonesha alizaliwa hospitali ya Ilala Oktoba 20, 1989.
Mwengine ni Godfrey Tide Sanga aliyezaliwa Arusha mwaka 1985, na ambaye alikuwa na pasi ya kusafiria ya Tanzania iliyotolewa tarehe 8 Septemba, 2011 mjini Dar es Salaam.
Mussa alisema, mtu huyo pia aliwasilisha vyeti vya masomo vinavyoonesha skuli mbalimbali alizosoma nchini, ingawa alisema kisheria hivyo si vielelezo vya kuthibitisha uraia wa mtu, lakini idara hiyo ilitosheka na pasi yake, ambayo asingeweza kuipata bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha alimtaja mtu mwengine kuwa ni Editha Ebehat Christom mkaazi wa Jang'ombe, ambaye aliwasilisha cheti cha kuzaliwa kinachoonesha kwamba alizaliwa Zanzibar tarehe 14 Mei, 1989.
Alieleza kuwa, mwanamke huyo pia alionesha kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi pamoja na baadhi ya maofisa wa idara hiyo kuthibitisha kwamba wanamfahamu vyema.
Watu wengine wawili ambao alisema idara yake inaendelea kuwachunguza ni Fatma Idrissa Hussein, ambaye alidai ni Mtanzania mzaliwa wa Kigoma na kwamba alikuweko Zanzibar kwa shughuli za biashara na hivyo alipewa muda akachukue vielelezo vyake.
Alimtaja mwengine kuwa ni Sadiki Aloyce Mwanjema, ambaye alionesha barua ya mahakama ya Kadhi Zanzibar ya tarehe 28 Novemba 2010, lakini akasema hicho si kielelezo cha kuthibitisha uraia wa mtu na ametakiwa apeleke nyaraka nyengine zilizo madhubuti.
Alipoulizwa iwapo watu hao wawili si raia wa Tanzania na kama watakapoondoka kufuata vielelezo vyao hawatarudi tena, Mwanasheria huyo alisema, kwa kufanya hivyo watakuwa wameisaidia idara yake kwa kuiepushia gharama za kuwarejesha walikotoka.
Alifahamisha kuwa kisheria, kazi ya kuwasaka watu wanaoshukiwa kuwa ni wahamiaji haramu ni ya jeshi la Polisi lakini idara yake ndiyo yenye jukumu la kuwachunguza kwa kuwahoji ili kubaini uraia wao.
Zanzibar Leo ilimpigia simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi kutaka maelezo kuhusu watu wengine watano waliotangaza kuwakamata katika operesheni ya kusaka wahamiaji haramu, lakini akasema suala hilo linamhusu Kamanda wa Polisi wilaya.
1 Comments
Hiliswala la kuwatafuta wahamiaji harumu ni lakupongeza kwa serekali, lakini, sheria hii ifanyekazi mpaka kwa wahamiaji haramu wa ndani ya nchi, hawa nao imekuwa tatizo, mfano, sheria, imeweka wazi, raia akihama mtaa kwenda mtaa, lazima afate taratibu, za kisheria, utona watu wanahama ovyo, kwenda mitaa mengine, bilakujali, harama, zakule aendako, titizo hili limejitokeza sana wakati wa uandishaji wapiga kura wapya, mtuanadai haki hali ya kuwamgeni, nimuhamiaji haram mtani na anadi atambuliwe na sheha, wakti alipo hamia haja fata shiria, zilizo panga na baraza lawakilish
ReplyDelete