Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki na Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Bibi Harriet Mathews,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,(katikati) ni Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki na Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Bibi Harriet Mathews,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,leo Mchana Mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Uingereza nchini Bibi Dianna Melrose
.[Picha na Ramadhan Othman.Ikulu.]
Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki na Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Bibi Harriet Mathews.
Mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Uingereza nchini Bibi Dianna Melrose yalihusu kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Uingereza.
Katika mazungumzo hayo Dk Shein ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa misaada yake kwa Zanzibar na kueleza matumaini yake kuendelea ushirikiano zaidi katika kusaidia Zanzibar kutimiza ndoto yake ya kuwa taifa lenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2020.
Alimueleza Bibi Mathews kuwa uwekezaji ni sehemu muhimu ya kupanua ushirikiano kati ya Uingereza na Zanzibar na kutoa wito kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo kuwekeza nchini hasa katika sekta ya Utalii na Uvuvi wa Bahari Kuu.
“Tuna fursa nyingi za uwekezaji ambazo sekta binafsi toka Uingereza inaweza kuwekeza. Kwa mfano tunahitaji wawekezaji wa daraja la juu katika sekta ya utalii ili waweze kujenga hoteli za kifahari za nyota tano” Dk. Shein alieleza.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo fursa katika sekta nyingi za uchumi lakini Dk. Shein alieleza kuwa sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni eneo ambalo likipata uwekezaji muafaka lina kila uwezo wa kubadili kabisa maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar.
“Bado hatujapata wawekezaji lakini uvuvi wa bahari kuu ni eneo ambalo linatupa matumaini makubwa endapo litapata uwekezaji mzuri” na kuongeza kuwa hiyo ni fursa nzuri kwa waingereza kuwekeza.
Dk. Shein alieleza kuwa eneo hilo linagusa maisha ya wananchi wengi na anaamini kuwa linaweza kusaidia kufikia malengo ya Serikali sio tu ya kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi wa nchi bali hata kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wa Zanzibar kwa kutoa ajira nyingi.
Kwa upande wake Bibi Harriet Mathews alisema Uingereza itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo ili kunyanyua kiwango cha maisha cha wananchi wake.
Bibi Mathews alibainisha kuwa Serikali ya nchi yake inaiona Zanzibar kuwa mshiriki muhimu katika mpango wa ushirikiano kati ya Uingereza na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kusaidia kufikia malengo yake maendeleo.
“Zanzibar ni mshiriki muhimu katika Mpango wetu wa Ushirikiano kati ya Uingereza na Afrika Mashariki ili hatimae iweze kufikia lengo lake la kuingia katika nchi zenye uchumi wa kipato cha kati”alisema Bibi Mathews.
0 Comments