Na Masanja Mabula, Pemba
MKUU wilaya ya Wete, Omar Khamis Othman, ameitaka jumuiya ya
madereva mkoa wa kaskazini Pemba kuwaelimisha madereva wa gari za abiria na
mizigo na wale wa vyombo vya maringi
mawili pamoja na abiria kufuata sheria
za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Alisema bado ajali nyingi za barabarani
zinazotokea husababishwa na madereva na abiria kutokana na kutozielewa vyema
sheria za barabarani.
Kauli hiyo aliitoa wakati akifunga kikao cha kutathimini hali
ya usafiri mkoa wa kaskazini Pemba kilichowashirikisha madereva, wamiliki wa
gari za abiria, wadau wa usafiri kutoka asasi za kiraia, jeshi la polisi na
watendaji kutoka Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano.
Alisema ni vyema pande hizo kushirikiana
pamoja kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wananchi ili waweze kuzielewa na
kuzifuata.
"Hili jambo linahitaji ushirikiano
wa pande zote, iwapo kila mmoja akiwajibika kwa mujibu wa nafasi yake tunaweza
kufanikisha kudhibiti ajali,” alisema.
Naye Mkuu wa Idara ya Leseni Pemba,
Khamis Ali Khatib, aliwataka wadau hao kushirikiana na kitengo hicho kwa
kuwafichua madereva ambao wamepata leseni za udereva lakini hawafuati taratibu.
Alisema taarifa hizo zitasaidia katika
kudhibiti ongezeko na ajali ambazo zinachangiwa na baadhi ya madereva wasiozingatia
sheria.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya madereva mkoa
huo, Tahir Omar Rehan, aliiomba serikali ya mkoa huo kuwashirikisha watendaji
wa jumuiya wakati wa kupanga gari ambazo zitashiriki katika masuala mbali mbali
ya kitaifa.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona kuna
gari zinatoka mkoa wa kusini Pemba kuja
kufanya kazi katika mkoa huo bila wao kujulishwa.
Kwa upande wake Ofisa Tawala Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Mwalimu Khamis Salim, ameitaka jumuiya hiyo na jeshi la polisi
kuendelea kuwaelimisha wananchi na kwamba serikali ya mkoa iko tayari kupokea
ushuri ili kufanikisha kupunguza ajali za barabarani.
0 Comments