Na Salim Said Salim
YAPO baadhi ya mambo yanapotokea hushangaza na kukufanya ujiulize masuala mengi, mojawapo ni ilikuwaje hata ikatokea ilivyotokea?
Miongoni mwa mambo yaliyonishangaza hivi karibuni ni kumsikia Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, akipiga marufuku maswali ya kibaguzi katika chombo hicho.
Kificho alitoa kauli hiyo baada kuulizwa swali kama upo mkataba wa Umoja wa Pemba na Unguja.
Pia alisikia kauli za kuwataka watu wa upande mmoja kuhama kwenda kwao.
Spika alirudia kauli ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mohammed Aboud (anatoka Pemba) ya kuwataka watu wa Pemba na Unguja kuishi kwa umoja, amani na utulivu na wawakilishi waache kuhoji mkataba wa Pemba na Unguja kwa kuwa haupo kwani Wazanzibari ni wamoja tangu asili.
Si ajabu ipo siku moja wawakilishi hawa watauliza mkataba wa Tumbatu na Makunduchi au Unguja mjini na mashamba au wa watu wanaoishi majirani mitaani na vijijini.
Sikushangazwa kusikia kauli hii ya kuulizia mkataba wa Unguja na Pemba katika Baraza la Wawakilishi kwa sababu hili sio suala lilioibuka sasa.
Nilieleza katika gazeti hili mwishoni mwa mwaka jana lilipoanzishwa kwa mara ya kwanza katika historia.
Waliofanya hivyo kumbukumbu zipo zinaonyesha kuwa ni wahafidhina wanaojiita wanachama kindaki ndaki wa CCM. Baadhi yao walitimuliwa serikalini kwa sababu ya jeuri, ujuba na nongwa zao kusababisha kufanya kazi ya fitna na uchochezi.
Wengine wanasemekana kununa, licha ya kuwa na umri mkubwa na kuanza kutumia mikongojo kwenda, kwa kutopewa vyeo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Lakini kwa mshangao wa wengi watu waliotoa kauli hizi za uchochezi hadharani hawakuwajibishwa kisheria. Hii ni wazi kuwa wana wa CCM, hata waseme nini hawahatarishi amani na utulivu.
Ninaamini kauli kama hizo za wahafidhina wa CCM zingelitoka mdomoni mwa wapinzani ndiyo ingekuwa nongwa na balaa isiyoelezeka.
Vipindi maalumu vingetayarishwa katika televisheni ya serikali (sio ya umma licha ya kuitwa ZBC) kuwalaani watu hao.
Jeshi la Polisi lingetoa taarifa kali na kuwafungulia mashitaka watu wanaosema hivyo kwa maelezo kuwa hawaitakii nchi mema, wamevunja katiba na sheria na wanahatarisha amani na utulivu uliopo nchini.
Kama wawakilishi wanaotunga sheria na kutarajiwa kuwa mfano mzuri wa kuziheshimu wanataka kuivigawa visiwa vya Unguja na Pemba, nini utarajie kwa mtu wa kawaida?
Labda wawakilishi wanafanya hivyo kwa sababu wanayo kinga ya kutoshitakiwa kwa wanayoyasema ndani ya Baraza.
Baraza linazo kanuni zake. Kwanini Spika Kificho asiwatoe ndani ya Baraza watu wa aina hii wanaotoa kauli zinazoweza kuwa cheche za kuwasha moto utakaokosa mzimaji?
Kwanza tulishuhudia Wapemba wakitengwa katika ajira za serikali na wengine (kwa mamia) kutimuliwa serikalini na kupoteza haki zao zote kutokana na hasira ya CCM kushindwa katika uchaguzi Pemba.
Hata mamia ya watoto wao walifukuzwa shule na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Omar Ramadhani Mapuri, na hawakufanya mtihani wa kidato cha sita kwa sababu walitaka kujiandikisha kuwa wapiga kura.
Mapuri, hakujua chuki zake kwa watoto wa Kipemba ndiyo ilikuwa kheri kwa baadhi yao ambao sasa ni walimu katika vyuo vikuu vya Ulaya na wengine ni madaktari, wahandisi katika nchi mbalimbali.
Kufukuzwa shule kuliwafungulia milango ya kwenda nje na kwa msaada wa jamaa zao, marafiki na jumuiya za kimataifa.
Unapokutana nao wanamshukuru Mapuri na kusema chuki zake ziliwafungulia mlango wa kheri na baraka.
Hata hivyo, sio vizuri kutarajia kauli kama hizi za kibaguzi za kutaka kuigawa Zanzibar zitaleta kheri. Nchi nyingi zilizovumilia watu waliopandikiza mbegu za chuki za watu kugawana zilijutia jambo hilo huku baadhi yao hadi leo hazikaliki.
Mchezo wa kuwafumbia macho watu wanaozusha ubaguzi, kama ule tuliokuwa tunaulaani Afrika Kusini hawafai kuvumiliwa.
Njia nzuri ya kuhakikisha nchi inatulia ni kuchukua hatua za kuwadhibiti, ikiwa pamoja na kuwawajibisha kisheria.
Lakini kwa vile wawakilishi kama ilivyo kwa wenzao wabunge wanayo kinga, ndiyo maana wanazungumza kadiri watakavyo. Naona ni vema vyama vyao vikawadhibiti, kuwakemea na kuwalaani.
Kitendo cha viongozi wakuu wa CCM kukaa kimya wakati kauli hizi zinatolewa, kunatoa tafsiri kwamba wametumwa kufanya hivyo na labda chama hicho katika kujipapatua kimeamua kuwa na siasa za kuigawa Zanzibar.
Ni kweli chama cha siasa lazima kiumie na kione uchungu kinapoona watu wa eneo moja la nchi hawakitaki na hawakipi kura katika uchaguzi.
Lakini hii haiwezi kuwa leseni ya kuzusha siasa za ubaguzi kwani na wapinzani hukosa kura katika baadhi ya maeneo ya nchi. Hii ndiyo siasa na kama CCM wanajidai wamebobea kwa siasa, basi hawakustahili kuonyesha chuki za aina hii kwa Wapemba.
Kwa kawaida kila mtu akiona unazidi kumchukia ndio huwa anakaza kamba ya kukuona hufai kushirikiana naye.
CCM inapaswa ijifunze ustahamilivu na kama kutumia matusi basi Wapemba wameshatukanwa vya kutosha na hata kuwaita vijibwa vya santuri.
Kama kuwapiga hilo wamelizoea na kama kutia kinyesi visima vyao hilo kwao ni kama kuwafukizia udi maji yao. Hata Rais mstaafu wa awamu ya tano, Salmin Amour, alisema hawataki Wapemba katika serikali yake na ndiyo maana aliwatimua waliokuwa wanashika nafasi za uongozi.
Lakini wakati alipofanya hivyo hakuwa na ubavu wa kukataa karafuu zinazotoka Pemba ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikichangia sehemu kubwa ya pato la Zanzibar.
Tabia ya Salmin ambaye alikuwa hafichi chuki zake kwa Wapemba (sijui wamemkosea nini au labda kwa sababu alipata asilimia 9 ya kura kutoka Pemba) ni kama ile wanayosema Waswahili kuwa “Baniani mbaya kiatu chake dawa”.
Ni vizuri kwa serikali kuchukua hatua za kuwadhibiti wahafidhina na wawakilishi wanaotoa kauli hizi za hatari. Tukumbuke wosia wa wahenga unaosema ‘nyimbo mbaya habembelezewi mtoto’.
Mchezo wa nalitote tugawane mbao hauna kheri. Watu huchezea mpira au gololi mchezo wanaoutaka na sio amani.
Kauli za kibaguzi huwa hazina kheri na hili tumeliona katika nchi nyingi. Ni vizuri tukajifunza, badala ya kusubitri ulimwengu utufunze.
Wazanzibari wanaowanyamazia wanaotaka kuwagawa waelewe wanavumilia uozo ambao maradhi yake ya kuambukiza si rahisi kutibika.
Kwa kawaida Wazanzibari wengi hutafuta kisingizio cha kudai ndugu zao wa Bara hawawatakii mema na ndio wanaopalilia chuki.
Lakini tunachokiona ni kuwa kisima cha kuwatumbukiza kwenye maovu kinachimbwa na wenyewe watu wa visiwani na kwa hili wasije kudai watu wa Bara ndio chanzo cha balaa inayoweza kuwakuta huko mbele.
Kuwavumilia wanaopalilia siasa za chuki na ubaguzi ni kujipalilia makaa kama afanyavyo pweza.
Sheria za kuwakabili wachochezi zipo. Ni vyema zikatumika, lakini ni kwa ajili ya wapinzani tu, basi ole wao Wazanzibari wote kwani balaa ikizuka haitachagua huyu ni CCM au yule ni mpinzani.
Chanzo - Tanzania Daima
0 Comments