Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Ali Mohammed Shein, amefanya uteuzi wa wajumbe
wa bodi katika taasisi mbali mbali za serikali.
Uteuzi huo ulitangazwa mjini
Zanzibar na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid
Yahya Mzee, ambapo alieleza kuwa ulianza rasmi Septemba 30 mwaka huu.
Walioteuliwa ni Dk. Issa Haji
Ziddy, anaekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni Wakfu na Mali ya Amana, ambapo
uteuzi huo umefanywa chini ya sheria namba 2 ya mwaka 2007 kifungu cha 5 (2)
iliyounda taasisi hiyo.
Kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu, Mwenyekiti anakuwa Kombo Hassan Juma, ambapo uteuzi wake umefanywa
chini ya sheria namba 3 ya mwaka 2011 kifungu cha 4 (1)(a).
Dk.Mohammed Mwinyi Mzale,
ameteuliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi (ZIPA) chini
ya sheria namba 11 ya mwaka 2004, kifungu cha 6(2) (a).
Kwa upande wa Shirika la Meli
na Uwakala chini ya sheria namba 3 ya mwaka 2013 kifungu cha 10 (2)(a),Dk
Shein, amemteua Kepteni, Abdulla Yussuf Jumbe, kuwa Mwenyekiti wa bodi ya shirika
hilo.
Kwa upande wa Mamlaka ya
Usafiri Baharini (ZMA), Dk. Shein amemteua, Ahmeid Sheikh Abdulrahman kuwa
Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo.
Bodi ya Ushauri ya Mambo ya
Nyaraka na Kumbukumbu, alieteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ni Amour Abdalla
Khamis.
Aidha alimteua Mwalimu Haji
Ameir, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na Salmin Senga Salmin kuwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari.
1 Comments
Walewale mpaka dunia imalizike. Hawa kina Senga na Jumbe wanakijua nini Dunia hii ya Sayansi na Teknolojia.
ReplyDelete