Na Khamis Amani
MAMLAKA ya Uwekezaji Vitega
Uchumi Zanzibar (ZIPA) imewaomba wafanyabiashara wa kigeni kuvitumia vizuri
vivutio vya Zanzibar kwa kuwekeza miradi yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA,Ndg. Salum Nassor, alisema Zanzibar ni visiwa vilivyojaaliwa kuwa na vivutio vingi
na vizuri kwa uwekezaji, ambavyo vinaweza kukuza biashara.
Aliyasema hayo katika hoteli ya
Double Tree Shangani mjini Unguja, wakati wa mkutano na wafanyabiashara wakubwa
kutoka nchini Marekani wa VIP Safari.
Alisema vivutio vya Zanzibar
vina mandhari nzuri kwa wawekezaji ambavyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza
biashara ikiwemo utalii.
Alisema ujio wa wafanyabiashara
hao utasaidia kuitangaza Zanzibar kiuchumi na kiutalii pamoja na kukuza urafiki
wa muda mrefu baina ya Tanzania na Marekani.
Hivyo aliwaomba wafanyabiashara
hao kukubali kuwekeza miradi yao ambayo itasaidia kuondoa umasikini kwa
kuwapatia ajira vijana, kuitangaza nchi pamoja na kuinua pato la taifa.
Balozi wa Tanzania mjini Washington
DC, Balozi. Suleiman Saleh, alisema Tanzania ni nchi iliyojaaliwa na vivutio vingi vya
utalii ikiwemo mbuga za wanyama na fukwe za bahari, ambazo vikitangazwa
vinaweza kuwashawishi wawekezaji kuwekeza miradi yao.
Alisema, ubalozi wake umefanya
jitihada kubwa za kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar kuvutia wawekezaji jambo
ambalo linahitaji kuungwa mkono na serikali na wadau wote wa utalii.
Alisema katika kufanikisha hilo
aliweza kuwafikisha wafanyabiashara wakubwa kukagua vivutio hivyo ambavyo
vimeleta mafanikio katika suala zima la uwekezaji.
Alisema ujio wa wafanyabiashara
hao unaweza kuleta tija katika sekta ya uwekezaji jambo ambalo linahitaji
jitihada za Serikali katika kuimarisha ulinzi kwa wawekezaji, watalii na mali
zao pamoja na kuweka miundombinu imara.
Nao wafanyabiashara hao
walisema, wameridhishwa na vivutio vizuri vilivyopo Zanzibar na kuahidi
kuwekeza miradi yao pamoja na kuitangaza nchi kiutalii.
Hiyo ni ziara ya tatu kwa
wafanyabiashara wakubwa wa Marekani kufika nchini kwa ajili ya kukagua vivutio
kwa ajili ya uwekezaji.
0 Comments