Na: A. Othman
Mshairi
nguli na mwalimu mzoefu wa Kiswahili ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe kutoka
nchini Kenya, Bwana Abdilatif Abdalla amemtembelea mwandishi chipukizi kutoka
Zanzibar, Bwana Yussuf Shoka ofisini kwake jijini London mapema wiki hii.
Katika ziara yake hiyo fupi Bwana Abdalla alifanya mazungumzo mafupi na
mwandishi huyo kuhusu kitabu chake kipya cha ‘Paka wa Binti Hatibu’.
Gwiji
huyo ambaye ametumia muda mwingi kufundisha Kiswahili nchini Uingereza na Leipzig,
Ujerumani amejinyakulia umaarufu mkubwa zaidi katika tasnia ya ushairi kwa kazi
yake iitwayo ‘Sauti ya dhiki’ (1973)’.Sambamba na kazi hiyo Bwana Abdilatif
Abdalla ambaye ni Profesa mstaafu wa chuo kikuu cha Leipzig Ujerumani, kwa sasa
amekuwa akitembelea sehemu mbali mbali duniani na kutoa mihadhara yake kufuatia
mialiko anayoipata.
Bwana
Abdalla alifika chuo kikuu cha London, SOAS majira ya mchana wa Jumatatu
(5-01-2015) na kukaribishwa na mkuu wa
Idara ya lugha na Tamaduni za Afrika ambaye pia ni mwalimu wa Fasihi ya
Kiswahili Chuoni hapo, Dr. Alena Rettova ambapo pia alikutana na kufanya mazungumzo
mafupi na Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili na Tafsiri wa chuo hicho Dr. Chege Githiora.
Katika
ziara yake hiyo fupi, Bwana Abdalla alikutanishwa na kutambulishwa kwa
mwandishi wa ‘Paka wa Binti Hatibu’ na mwenyeji wake Dr. Rettova ambapo kimsingi
mwalimu huyo alitaka kujua kwa kina fasili ya msemo huo na jinsi mwandishi huyo
alivyoutumia katika kazi yake hiyo ya sanaa.
Naye,
Mwandishi wa kitabu hicho ambaye pia ni mwalimu wa lugha na Fasihi chuoni hapo,
Bwana Yussuf Shoka alijadiliana na mtaalamu huyo kwa kina juu ya fasili ya
msemo huo na kuhitimisha kwa kusema;
‘Unajua
katika utangulizi wa kitabu hiki, mwandishi wa utangulizi Bi Asha Khamis Hamad
amesema – ukitaka kujua uhondo wa ngoma ingia ucheze, na ukitaka kujua uhondo
wa kitabu hiki kisome’.
Wakati
huo huo, Bwana Abdilatif Abdalla alitumia fursa hiyo kumshauri mwandishi huyo
chipukizi kuandika kwa kutumia lugha yake ya kawaida yaani lugha ya
kimazungumzo:
‘Hakuna
haja ya kung’ang’ania usanifu. Andika Kiswahili unachokizungumza katika
mazingira ya kawaida. Kiswahili unachozungumza nyumbani na watu wako’.
Akiongezea na kutetea hoja yake, Bwana Abdalla alitoa mfano wa Profesa Said Ahmed Muhammed kwa kusema;
‘Watu
wengi wanashindwa kufahamu uandishi wa Said Ahmed eti kwa sababu anaandika kwa
lugha ya kawaida. Lugha ya kwao. Nami siku zote humwambia endelea kuandika hivyo
hivyo, kwani hicho ndicho Kiswahili kinachotumiwa na watu wako.’
Bwana
Abdalla pia alimalizia kwa kusema kuwa Kiswahili kimekuwa lugha ya watu wote.
Hivyo hakuna haja ya kusema huyu hivi na huyu vile kwani wenye lugha ni watumiaji wa lugha yenyewe.
Mwandishi
huyo pia atatembelewa na mwalimu mkongwe na gwiji wa uandishi wa tamthiliya za
Kiswahili visiwani Zanzibar, Bwana Farouk Topan mapema wiki hii. Bwana Topan ni
profesa mstaafu wa Kiswahili wa chuo kikuu cha London, SOAS ambaye anajulikana
zaidi kwa kazi zake za sanaa ya maigizo kama vile Mfalme Juha (1971), Aliyeonja
Pepo (1973) na Siri (2000).
0 Comments