Hayo yamesemwa na Makmu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Mahafali ya 13 ya Zanzibar School of Health yaliyofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Mao Zedong Wilaya ya Mjini Unguja.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu mbali mbali ya Afya ikiwemo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na maslahi ya watumishi ili kuongeza ari katika utumishi wao.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imepanga kuajiri watumishi wa Sekta ya Afya 1,566 ili kuongeza kasi ya utoaji wa huduma mijini na vijijini.
Amesema kuwa Serikali imeongeza ufadhili kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu kutoka idadi ya wanafunzi 8,870 kwa mwaka 2024 hadi wanafunzi elf 20 ambapo amewataka wahitimu hao kuitumia fursa hio kwa kujiendeleza kielimu ili waweze kufikia ngazi ya ubingwa na ubingwa ubobezi katika kada zao.
Amewasihi wahitimu hao kujenga utayari wa kiutumishi, kushirikiana na wengine katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuzingatia misingi ya uadilifu heshima, huruma na utu kwa kufuata kanuni za taaluma yao zitakowaepusha na mambo yote ambayo yanadhalilisha taaluma ya afya.
Mhe. Hemed ameutaka uongozi wa Zanzibar School of Health kuendelea kusimamia ubora wa elimu, kufanya tafiti, kuwaendeleza kielimu wafanyakazi waliopo kazini na kuandaa kozi nyengine muhimu kwa Taifa kama ambavyo wametangaza kuanzisha kozi ya Maabara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano utakaohitajika ili kuhakikisha chuo hicho na vyuo vyengine nchini linaendelea kuimarika na kuzalisha wataalamu wa fani mbali mbali wakaolitumikia Taifa mara baada ya kumaliza masomo yao.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema Wizara ya elimu ipo tayari kufanya kazi na Uongozi wa Zanzibar School of Health (ZSH) katika kuhakikisha chuo hicho kinaendela kutoa taaluma bora za kada ya Afya kwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo .
Waziri Lela amefahamisha kuwa kumekuwa na uhaba mkubwa wa watumishi katika sekta ya Afya hivyo chuo cha Zanzibar School of Health kina fursa ya kuendelea kuanzisha kozi mbali mbali za kipaombele katika sekta ya Afya ili kukidhi uhitaji uliopo sasa.
Mhe. Lela ameupongeza Uongozi wa Zanzibar School of Health kwa kuendelea kuwa chuo bora kinachotoa wahitimu wengi wenye sifa na utayari wa kuitumikia nchi.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake mwanafunzi Is-haka Sliim Yahya amewashukuru walimu na Uongozi mzima wa Zanzibar School of Health kwa kuwasomesha na kuwalea katika malezi bora yaliyowajenga kuwa na utayari wa kufanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii kwa uweledi na maadili mema.
Wahitimu hao wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuipa kipaombele Sekta ya elimu kwa kuongeza Bajeti ya Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu ambayo imewaondolea wanafunzi wengi changamoto ya Ada kwa kupatiwa mikopo inayowasaidia kusoma pasipo na usumbufu wa aina yoyote.
Wamesema wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali wanapokuwa katika mafunzo yao kwa vitendo ikiwa ni paoja na kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi hasa katika hospitali za umma na kutokuwepo kwa watumishi maalum wakuwafundisha na kuwaongoza hivyo wameiomba Serikali pamoja na Uongozi wa Chuo hicho kuiangalia kwa umakini changamoto hizo ambazo zinazorotesha upatikanaji wa taaluma kwa wanfunzi hao.
Wahitimu hao Wameahidi kufanya kazi kwa heshima na nidhamu, kufuata miiko na maadili ya kazi zao na kuzitumia vyema taaluma zao kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa na jamii kwa ujumla.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 06 / 12 / 2025.
0 Comments