6/recent/ticker-posts

"EPUKENI KUFANYA KAZI KWA KUSUKUMWA NA MASLAHI BINAFSI" NAIBU WAZIRI KASPAR MMUYA

Naibu Waziri wa Ardhi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akimkabidhi tuzo Mthamini Mkuu ya kutambua umahiri wa usimamizi wa Wathamini FRV  Evelyne Mugasha wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Mwaka Bodi ya Usajili ya Wathamini (VRB) uliofanyika kuanzia Desemba 4 hadi 5, 2025 mkoani Morogoro. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara Ardhi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera.

Na Eleuteri Mangi, Morogoro.

Naibu Waziri wa Ardhi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesisitiza Wataalamu wa Uthamini nchini kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya taaluma zao ili kuepuka kufanya kazi kwa kusukumwa na maslahi binafsi.

Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya amesema hayo kwa niaba ya Waziri wa Ardhi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa sita wa Mwaka Bodi ya Usajili ya Wathamini (VRB) uliofanyika mkoani Morogoro kuanzia Desemba 4 hadi 5, 2025.

Ili kufikia malengo hayo, Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya amesistiza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa na kutekeleza mpango wa mafunzo endelevu ya matumizi ya teknolojia na mabadiliko yake ya mara kwa mara katika kazi za kila siku ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia katika kutekeleza majukumu yao na kuwahudumia wananchi kwa wakati katika sekta ya ardhi.

Mhe. Mmuya amewasisitiza Wathamini kutenda haki wanapotekeleza majukumu yao ikiwa ni kutafsiri kwa vitendo dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanya kazi kwa kuzingatia utu.

"Tutende haki kwa watu wetu tunaowasimamia na kama hufanyi vema kwa wale unaowasimamia thamani yako wewe kwao iko wapi? Wathamini wote mnapofanya kazi zenu zingatieni thamani halisi ya mali inayothaminiwa tofauti na hivyo kupoteza uhalali wa kazi zenu, imani ya wadau wenu, mapato ya serikali lakini pia kuwanyima haki wale wanaostahili kupata haki stahiki kwa mali zao" amesisitiza Naibu Waziri Mmuya.

Aidha, Naibu Waziri Mhe. Mmuya ameagiza Wizara hiyo Ishirikiane na wathamini wa sekta binafsi kufanya kazi za uthamini na kutumia fursa ya uwepo wa wathamini binafsi katika kutoa huduma kwa kuzingatia Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inasisitiza sana ushirikiano na sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa.

Pia amewataka Wathamini wanapotekeleza majukumu yao kulinda mazingira na rasilimali za asili kwa kuzingatia athari za kimazingira, ufanisi wa nishati, maendelezo ya kijani na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi na kwa kuhimiza mbinu endelevu, na kuhakikisha thamani ya ardhi na mali inajumuisha pia urithi wa asili kwa maendeleo ya Taifa.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mhe. Kaspar kufungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Bi. Lucy Kabyemera amesema Wathamini wamepokea vizuri Mfumo wa e-Ardhi na wanautumia ambao ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwahudumia wananchi kupitia mifumo ili kurahisisha utoaji wa huduma za ardhi kote nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili ya Wathamini Bw. Zidikheri Mgaya Mudeme amesema ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Wathamini wote wa Serikali na sekta binafsi kwa kuwa wanawajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya taifa na kuwahudumia watanzania kwenye sekta ya Uthamini na kuongeza kuwa mikutano hiyo imekua nyenzo nzuri ya kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Naibu Waziri wa Ardhi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akifungua Mkutano Mkuu wa sita wa Mwaka Bodi ya Usajili ya Wathamini (VRB) uliofanyika kuanzia Desemba 4 hadi 5, 2025 mkoani Morogoro.


Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa sita wa Mwaka Bodi ya Usajili ya Wathamini (VRB) wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika kuanzia Desemba 4 hadi 5, 2025 mkoani Morogoro.


 

Post a Comment

0 Comments