6/recent/ticker-posts

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Ameshiriki Bonaza la Mazoezi ya Viungo Mkoa wa Kaskazini Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.  Hemed Suleiman Abdulla akiongoza matembezi na  Bonanza la mazoezi ya viungo lililoandawa na wanamichezo wa Zone "C" na kufanyika katika kijiji cha Kinduni Mkoa wa Kaskazi Unguja.

Wananchi wamehimizwa kuendelea kufanya mazoezi ili kuboresha afya ya  mwili na kujiepusha na maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, sindikizo la damu na mengineyo.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Bonanza la mchezo wa mazoezi ya viungo la zone "C" lililofanyika katika kijiji cha Kinduni Mkoa wa Kaskazi Unguja.

Amesema kufanya mazoezi ya viongo kwa pamoja huimarisha zaidi afya ya mwili na akili pia hujenga umoja, upendo na mshikamano katika jamii zetu. 

Mhe. Hemed  amefahamisha kuwa kufanya mazoezi ipasavyo kunasaidia kupunguza uzito na mafuta mwilini ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari, sindikizo la damu na magojwa ya moyo jambo ambalo linaweza kuepukika endapo wananchi watajenga tabia ya kufanya mazoezi na kujiepusha na ulaji mbaya wa chakula.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano katika kuhakikisha sekta ya Michezo inaimarika zaidi na kutoa faida chanya kwa wanamichezo na wananchi kwa ujumla.

Mhe. Hemed ameitaka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuwa  tayari kushirikiana  na ZABESA kwa kuwapatia fursa za kujiendeleza kielimu walimu wa mazoezi ambao watakuwa na uwezo wa kufanyisha wanamichezo mazoezi kwa uweledi na umakini zaidi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wanamichezo na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji kama vile  wanaofanyiwa upasuaji, waathirika wa ajali, akina mama wanaopoteza damu  wakati wa kujifungua na wagonjwa wenye magonjwa yanayohitaji damu mara kwa mara).

Katika Bonanza hilo, Mhe.Hemed amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini na kujiepusha na kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kupiteza Amani iliopo nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe.  Riziki Pembe Juma amekishukuru chama cha Mchezo wa viungo Zanzibar (ZABESA) kwa kuendelea kushirikiana na wizara ya habari katika kuhamasisha na kuelimisha wananchi umuhimu wa kufanya mazoezi kwa maendeleo ya Taifa na afya zao kwa ujumla.

Mhe. Pembe amewataka wazanzibari kujenga utamaduni wa kuhamasishana  kufanya mazoezi kwa rika zote ili kulinda afya zao na magonjwa nyemelezi ambayo yamekuwa yakiwakumba wananchi wengi kutokana na kutokufanya mazoezi.

Akisoma risala kwa niaba ya wanamichezo wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mwenyekiti wa chama cha mazoezi ya Viungo Zone "C" ndugu Amour Hamad Amour amesema wanamichezo wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi na wako tayari wakati wowote kutoa ushirikiano katika ujenzi wa Taifa.

Mwenyekiti Amour ametoa wito kwa wanamichezo na wananchi wa Kaskazi Unguja mara baada ya kumalizika kwa Bonanza hilo kujitokeza kupima afya zao na kuchangia damu ili kusaidia wananchi wenye uhitaji.

Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe  07 / 12 / 2025

Post a Comment

0 Comments