Na.Omar Abdallah -Wizara ya Afya Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya Zanzibar imeendelea kutoa vipaumbele katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha mahitaji ya msingi ya afya yanaendana na mpango kazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO).Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya pamoja kati ya Serikali na Shirika hilo la kimataifa.
Akizungumza katika mkutano wa mashirikiaono ya Wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wa kujadili vipao mbele vya Afya Zanzibar Msimamizi wa ofisi ya WHO Zanzibar Dr Nemes Iriya amesema kwa kawaida, mpango kazi wa WHO huandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na serikali za nchi wanachama ili kuhakikisha mipango hiyo inaendana na vipaumbele vya kitaifa.
Katika kikao kilichofanyika na wadau wa sekta ya afya wamekutana
kupitia mpango wa WHO unaotekelezwa duniani na kuulinganisha na maeneo ya
kipaumbele yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wadau wametathmini namna mpango wa kimataifa unavyoweza
kuakisi mahitaji halisi ya Zanzibar, ili kuuwezesha kuingizwa kwa ufanisi
katika mpango wa pamoja wa utekelezaji.
Aidha, imeelezwa kuwa vigezo vya maendeleo katika sekta ya
afya vinapaswa kuendana na mkakati wa Wizara ya Afya pamoja na miongozo ya
Serikali, huku baadhi ya vigezo vikionekana kutofautiana na vile vya mpango wa
kimataifa.
Kupitia majadiliano hayo, Serikali ya Zanzibar na WHO
wamekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa karibu katika kuratibu na kuoanisha
vigezo hivyo, ili kuhakikisha vinakidhi malengo yaliyopangwa na pande zote
mbili.
Mpango huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, sambamba na kuimarisha uwezo wa Serikali katika kufikia viwango vya kimataifa vya maendeleo ya afya.
Mkurugenzi Sera mipango
na utafiti Wizara ya Afya Zanzibar
Abdul Latif Khatib Haji
Amesema Lengo la kikao hicho ni kupitia taarifa kutoka
Vitengo na programu husika, ili kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha utoaji
wa huduma za afya.
Aidha Amesema Kupitia majadiliano hayo, wizara imepanga
kuandaa Mpango Mkakati wa Muda wa Kati ambao utaainisha maeneo ya kipaumbele
yatakayochochea uimarishaji wa huduma za afya kwa wananchi. Mpango huo wa miaka
miwili unatarajiwa kuanza mnao mwezi
julai 2026 hadi mwaka 2028 kuwa na hatua
mahsusi zitakazosaidia kuongeza ufanisi, kuboresha miundombinu, na kuimarisha
huduma za afya kwa ujumla.
Wizara inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama, sambamba na kutimiza dira na maelekezo ya Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini.
Nae Mkuu wa kitengo cha maradhi yasiombukiza Zanzibar Dr
Omar Mohammed Amesema wadau wa Vitengo mbalimbali wamewasilisha maoni yao miongoni vipaumbele vya sasa ni pamoja na
magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) pamoja na
huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Maeneo haya yameonekana kuhitaji nguvu ya pamoja kwani
yanagusa maisha ya watu wengi, hususan katika jamii zinazokaa mbali na vituo
vikuu vya huduma.
Wadau hao wameeleza kuwa changamoto hizi haziwezi
kutatuliwa kwa upande mmoja pekee, bali zinahitaji ushirikiano wa sekta
mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa.
MWISHO.
0 Comments