Wizara ya Afya Zanzibar inakusudia kufanya tathmini ya mwenendo wa maradhi ya macho hapa nchini kwa shehia 69 kwa Unguja na Pemba na utashirikisha watu kuanzia miaka 50 na kuendelea ili kuweza kupanga mikakati wa utoaji wa huduma za afya ya macho.
Akizungumzia tathmini hiyo Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema katika kukabiliana na maradhi ya macho Wizara ya Afya kwa kushirikina na wadau mbali mbali wameona ipo haja ya kufanya utafiti ambao utaonesha ukubwa wa tatizo na kuweza kuimarisha huduma katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Amefahamisha kuwa Zanzibar kama nchi nyengine itahakikisha inakabiliaana na tatizo la upofu, kupitia mikakati na tafiti maalumu zinazotekelezwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Amesema kuwa matatizo mingi yanayosababisha shida ya macho yanazuilika na amesema kuwa wizara ya afya inaendelea kuweka mikakati endelevu ya kupunguza vyanzo vya upofu vinavyoweza kuzuilika.
Nae mratibu wa huduma za afya ya macho Zanzibar Dkt. Fatma Juma Omar amesema wanatarajia tathmini hiyo itaisaidia wizara ya afya kupanga mikakati yake ya kukabiliana na matatizo ya macho yanayoweza kuzuilika ili kupunguza upofu hapa Zanzibar.
Amesisitiza kuwa changamoto zinazotokana na maradhi kama kisukari na shinikizo la damu nazo zimeendelea kuwa miongoni mwa sababu zinazoathiri uwezo wa kuona, hivyo ufuatiliaji wa karibu na elimu ya kinga ni muhimu kwa jamii.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo ya ufanyaji wa tathmini hiyo wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutambua visababishi vya upofu na kuendelea kuisaidia jamii ya Wazee wa Zanzibar kuondokana na tatizo hilo.
Tathimini hii hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo jumla ya watu elfu nne watafikiwa na tathmini hii unguja na pemba ili kupata takwimu zitakazosaidia kupanga mikakati mipya yenye lengo la kuzuia wananchi kupata upofu.
Mwisho.
.jpg)
0 Comments