6/recent/ticker-posts

ASKARI WA KIKE MKOA WA SONGWE WATAKIWA KUWA MFANO BORA NDANI NA NJE YA JESHI.

Na Issa Mwadangala.

Katibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pili Mande amewataka askari wa kike mkoani Songwe kuimarisha mshikamano, kushirikiana na kuwa kioo cha jamii katika nyanja mbalimbali, hususan kwenye masuala ya kijamii na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Wito huo umetolewa Januari 20, 2026 katika ukumbi wa Polisi Vwawa uliopo Wilaya ya Mbozi, ambapo SACP Mande amesisitiza umuhimu wa askari wa kike kuendeleza maadili mema, kulinda amani, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii hata nje ya majukumu yao ya kazi ili kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na jamii.

Aidha, SACP Mande amesema tangu kuanzishwa kwa Mtandao wa Polisi Wanawake mwaka 2007, umepata mafanikio makubwa ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu ili kulifanya Jeshi la Polisi kuwa jirani na rafiki wa jamii.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi Wilfred Willa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma, Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, amesema ustawi wa askari wa kike unapimwa kwa nidhamu na weledi kazini na nje ya kazi, hivyo amewahimiza kuendelea kutoa huduma bora na kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii ili kulinda taswira chanya ya Jeshi la Polisi.









Post a Comment

0 Comments