Mkurugenzi Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Msafiri Marijani amefanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Mkoa wa Lumumba na Hospitali ya Wilaya Ijitimai na Chumbuni kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma za afya pamoja na kufuatilia kwa karibu namna kampuni ya Seifee inavyotekeleza majukumu yake ndani ya hospitali za Wilaya.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali hizo Dkt Marijani amesema kuwa miongoni mwa mkakati wa Wizara ya Afya kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa zenye ubora na zenye kuzingatia viwango vilivyowekwa na Serikali.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kubaini changamoto katika maeneo yao na yanayohitaji kuimarishwa yafanyike mapema ili lengo la wananchi kupata huduma zenye ubora lifanikiwe.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Tiba alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali ikiwemo wodi za wagonjwa, maabara, huduma za dharura na alionesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa, huku akisisitiza umuhimu kuimarisha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amefahamisha kuwa katika ziara hiyo amebaini changamoto mbali mbali ikiwemo uhaba wa nafasi ya utoaji wa huduma zikiwemo za masikio koo na pua, uchakavu wa vifaa pamoja na kuzidiwa kwa wagonjwa waliofika kupata huduma kwa kulazwa kitanda kimoja zaidi ya mgonjwa mmoja.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya inafanya jitihada kubwa ya kujenga vituo vya Afya katika maeneo mbali mbali ili kupunguza mzigo wa watu wanaofika kupata huduma katika Hospitali za Wilaya.
Kwa upande wake Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya Chumbuni Antony Batazai Ngoi amesema kuwa katika ziara hiyo kumebainika na changamoto mbali mbali ikiwemo ya mfumo wa mtandao jambo ambalo limepelekea kudhorotesha baadhi ya huduma na kusababisha wagonjwa kusubiria kwa muda mrefu.
Aidha amefahamisha kuwa katika kuimarisha huduma za Afya watashirikiana na Kampuni ya Saifee kutatua changamoto zote za upatikanaji wa huduma ikiwemo mifumo ili wananchi wapate huduma zenye ubora.


0 Comments