NA Ali Abass, SCCM
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, kipo tayari kushirikiana na Chuo cha Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali ( DTI), kuanzisha mitaala ya kozi za akili mnemba (Artificial interligence) ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa ajira kwa vijana nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof.Abdi Talib Abdalla, wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe kutoka Chuo cha DTI , uliofika Makao Makuu ya SUZA,Tunguu, Mkoa wa Kusini, Unguja ili kujadili namna ya Chuo cha SUZA na Chuo huo hicho vitakavyo shirikiana kuanzisha kozi hiyo kwa pamoja.
Prof. Abdi ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, alieleza kuwa, SUZA ina wataalamu wenye sifa na rasilimali za kutosha za kuendeshea programu hiyo ikiwemo Majengo , hivyo ameutowa wasi wasi ujumbe huo kuwa SUZA haitarudi nyuma kushirikiana kuhakikisha malengo na mashirikiano yaliokusudiwa yanatimia.
Alisema mafunzo hayo yatasaidia vijana wengi wa Tanzania kuwa na ushindani katika soko la ajira, ambapo ,mafunzo hayo yanalega zaidi kutolewa kwa vitendo hali itakayo wasaidia kuwa na ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
“hapa hatuwafundishi wanafunzi nadharia lakini watafundishwa kufanya mambo kwa vitendo amabayo yanahusiana na teknolojia hii ya akili mnemba” alifahamisha Prof. Abdi.
Aidha aliuomba Uongozi wa Chuo hicho kufikiria kuanzisha Kampasi yake ndani ya eneo la Chuo Kikuu cha SUZA, ili kuendeleza mashirikiano ya karibu pindi Chuo hicho kitakapo kamilika.
“Tuna eneo la kutosha hapa ningefurahi zaidi kama mngeweza kufikiria namna ya kujenga jengo la kampasi ya chuo chenu ili tushirikiane kwa karibu zaidi” alisema
Naye Mwenyekiti wa Mradi wa DTI kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia Dkt. Ali Simba alisema, wamefika chuoni hapo kujiridhisha na utayari wa SUZA, katika maandalizi, ikiwemo Maabara zitakazo weza kupokea vifaa vya kuendeshea program hiyo na kufanya maandalizi ya kuanza kufundisha mitaala ya chuo cha taasisi ya taifa ya teknolojia ya kidijitali.
Alisema kuwa taasisi hiyo imeanzishwa kutokana na maono ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kuwasaidia vijana wa Tanzania kupata taaluma hiyo hapa nchini itakayo endana na na mabadiliko ya kidijitali.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Tanzania Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuhakikisha vijana wote wa kitanzania wenye elimu tofauti, kuweza kupatiwa mafunzo yatakayo wasaidia kuajiriwa na kujiajiri.
Alifahamisha kuwa Chuo hicho, kipo katika hatua za awali za ujenzi Mkoani Dodoma, ambapo kwa hatua za awali chuo hicho kitaanza kufundisha kozi zake kwa mashirikiano ya vyuo vikuu vya SUZA, MUST, UDSM na UDOM hadi pale hatua za ujenzi wa chuo hicho utakapo kamilika.
“Mtaala wa vyuo vyote hivi ni mmoja ila vitafundisha kozi tofauti, kwa mfano kwa SUZA, watafundisha kozi ya Akili Mnemba (AI), UDOM, watafundisha cyber security, MUST watafundisha, Big data and machine learning, UDSM watafundisha Internent of think (IOT)” alieleza Mawamgugu.


0 Comments