6/recent/ticker-posts

Taarifa ya Polisi kuelekea mchezo wa Young Africans na Al Ahly

 TAARIFA KWA UMMA 

KUELEKEA MCHEZO WA KIMATAIFA KATI YA 

YOUNG AFRICANS SC Vs AL AHLY YA NCHINI MISRI


Siku ya Jumamosi, tarehe 31 Januari 2026 kutakuwa na mchezo wa kimataifa wa mpira wa miguu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), mchezo huo utahusisha timu ya YOUNG AFRICANS SC ya Tanzania dhidi ya AL AHLY kutoka nchini Misri, ambapo mchezo huo utachezwa katika uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Kuelekea mchezo huo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tutahakikisha ulinzi unaimarishwa kipindi chote kabla, wakati na baada ya mchezo huo. 

Jeshi la Polisi linatambua kwamba mchezo huo ni mkubwa na unajenga heshima ya nchi yetu. Hivyo tutahakikisha tunasimamia kikamilifu hali ya usalama ili kuhakikisha hakuna vitendo vyenye kuleta uvunjifu wa amani kwa namna yeyote. Tutahakikisha kwamba wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu wanashiriki katika mchezo huo kwa usalama na amani.

Aidha, linatoa wito kwa wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira kuwahi kufika uwanjani mapema ili kuepuka msongamano na hakutoruhusiwa kuingia uwanjani na vitu hatarishi kama vile silaha.

Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote chenye lengo la kutumia mchezo huo kama fursa ya kufanya vitendo vya aina yeyote vinavyoenda kinyume na sheria na kwamba tumejipanga vizuri na tutahakikisha tunashughulika nao kwa mujibu wa sheria.

Onyo kwa madereva wa vyombo vya moto kutotumia mchezo huo kuwa sehemu ya kuvunja na kutotii sheria za usalama barabarani, kwani kutakuwa na idadi kubwa ya Askari wa Usalama barabarani na hatua kali za kisheria zitachukulia kwa yeyote atakayebainika kuendesha chombo cha moto kinyume na sheria.

Imetolewa na;

Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Mjini Magharibi.


Post a Comment

0 Comments