Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Ndg. Sultan Said Suleiman, amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na uaminifu kwa kuiga mifano ya wafanyakazi waliotangulia ambao wameacha alama ya utendaji bora, sambamba na kuimarisha uzalendo na ushirikiano mahali pa kazi.
Ndg. Sultan ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumuaga mfanyakazi wa Shirika la Nyumba aliyestaafu kutoka kada ya Masjala, Bi Mkubwa Sururu Shaaban, iliyofanyika katika Ofisi za ZHC, Darajani Zanzibar.
Amesema Shirika litaendelea kuthamini na kutambua mchango wa Bi Mkubwa katika kipindi chote cha utumishi wake, akieleza kuwa jitihada zake zimekuwa sehemu ya chachu ya maendeleo na mafanikio ya Shirika.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu alimkabidhi Bi Mkubwa zawadi maalum kama ishara ya upendo na shukrani kutoka kwa familia ya ZHC, zikiwemo pikipiki aina ya TVS kwa ajili ya shughuli za kujipatia kipato pamoja na vifaa vingine.
Kwa upande wake, mstaafu Bi Mkubwa Sururu Shaaban ameeleza kufurahishwa na namna Uongozi na wafanyakazi wa ZHC wanavyothamini na kujali ustawi wa watumishi wao, huku akitoa wito kwa wafanyakazi wanaoendelea na utumishi wa serikali kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, bidii na kujituma ili kuunga mkono jitihada za kuliimarisha Shirika la Nyumba Zanzibar.
Nao wafanyakazi wa ZHC wamemtakia heri na afya njema katika maisha yake mapya baada ya kustaafu, wakimuahidi kuendelea kushirikiana naye katika shida na raha kama sehemu ya familia ya Shirika la Nyumba Zanzibar.


0 Comments