6/recent/ticker-posts

DKT. MWIGULU: SERIKALI KUWAWEZESHA MAENEO NA MIKOPO WAMACHINGA, MAMA LISHE, BODABODA NA BAJAJI ● Serikali haitarajii wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo yasiyo na wateja

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemmba akizungumza na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima  (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka katika Kongamano la Mwaka la Wamachinga na Madereva wa Pikipiki na Bajaji za Kubeba Abiria lililohutubiwa na Waziri Mkuu kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa  cha Julius Nyerere jijini Dar eś salaam,


Serikali imejipanga kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wakiwemo wamachinga, mama lishe, madereva wa pikipiki (bodaboda) na bajaji, kwa kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyia biashara, mikopo nafuu na uratibu wa karibu wa kiserikali.

Hatua hiyo inalenga kuyatambua makundi hayo kama sehemu muhimu ya uchumi wa Taifa, kwa kuwawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira ya utulivu, usalama na tija, sambamba na mchango wao mkubwa katika utoaji wa ajira na huduma kwa wananchi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa kauli hiyo leo, Januari 08, 2026, alipokuwa akizungumza na wamachinga, mama lishe pamoja na madereva wa bodaboda na bajaji katika kongamano la mwaka lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imezipokea rasmi hoja zote zilizowasilishwa na wadau wa makundi hayo na kuzihakikishia kuwa zitafanyiwa kazi kwa vitendo, akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanaendesha shughuli zao bila usumbufu na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa Serikali haitarajii wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo yasiyo na wateja, akieleza kuwa itaendelea kushirikiana na viongozi wa makundi husika pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa kubainisha maeneo yanayofaa kwa shughuli zao. Ameongeza kuwa pale changamoto zitakapozidi uwezo wa mamlaka za chini, Serikali Kuu itaingilia kati ili kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana.

Aidha, amesema Serikali itaongeza fedha katika mfuko wa mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, sambamba na kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na maeneo rasmi ya kufanyia biashara, hatua itakayowawezesha wafanyabiashara wadogo na wasafirishaji kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na hadhi inayostahili.

Waziri Mkuu pia ametoa onyo kwa watendaji wa Serikali wanaotumia vibaya mamlaka yao kwa kujinufaisha kupitia maeneo ya wafanyabiashara, akisisitiza kuwa vitendo vya rushwa, unyonyaji na upangishaji holela wa maeneo havitavumiliwa.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili wafanyabiashara wadogo, madereva wa bodaboda na bajaji wachangamkie fursa mbalimbali za ajira, mikataba na biashara zinazopatikana ndani na nje ya nchi, huku sekta hizo zikiendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.

Vilevile, Dkt. Mwigulu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani aliweka utaratibu wa kuendesha Serikali kwa haki na kuwajali Watanzania, bila matumizi ya fedha za dhuluma. Ameeleza kuwa Rais aliielekeza Mamlaka ya Mapato kukusanya mapato kwa haki, na kwamba katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de Change), fedha zilizochukuliwa kwa makadirio yasiyo sahihi zilirejeshwa kwa wahusika, hatua iliyodhihirisha dhamira ya Serikali katika kulinda haki, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma.

(Mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JANUARI 08, 2026

Post a Comment

0 Comments